Huko kwenye kuogelea kimenuka

Monday March 5 2018

 

SI unakumbuka aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe alivyong’olewa madarakani, sasa unaambiwa mapinduzi kama hayo usishangae kuyaona yakifanyika kwenye Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA).

Wakati mambo yakionekana kuwa shwari, Mwanaspoti limebaini kuwa Rais wa TSA, Alex Mosha na Katibu Mkuu, Ramadhan Namkoveka wanaundiwa ‘zengwe’ la kung’olewa madarakani.

Ingawa katibu mkuu, Namkoveka amekanusha vikali hakuna kitu kama hicho, lakini Mwanaspoti limeshuhudia mkutano maalumu wa wajumbe wa mkutano mkuu ukiweka mikakati hiyo hivi karibu.

Mkutano huo ambao uliwajumuisha zaidi ya wajumbe 20 ulifanyika kwenye ukumbi wa Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST).

Ingawa Mosha na Namkoveka walishiriki katika hafla iliyoandaliwa na balozi wa Australia nchini hivi karibuni ya kuwaaga wanamichezo wanaokwenda kwenye mashindano ya Jumuiya ya Madola, habari za ndani zinabainisha kuwa tayari wamepinduliwa madarakani.

Wadau wa kuogelea wamebainisha moja ya sababu za kutaka kufanya mapinduzi hayo ni kutokana na rais wa TSA, Mosha kutamka Tanzania haiwezi kuleta medali ya kuogelea kwenye michezo ya mwaka huu ya Madola kule Australia.

Kauli hiyo ilitumiwa na Serikali na TOC kuwaengua waogeleaji Collins Saliboko na Selina Itatiro kushiriki michezo hiyo kwa kile walichosema hawawezi kupeleka ‘watalii’ kitendo ambacho kiliwachukiza wajumbe wa mkutano mkuu na kuanza harakati za kuwapindua madarakani.

Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja alikiri kupata taarifa za mgogoro huo.

“Kuna maelekezo nimewapa ambayo wanapaswa kuyafanya kwanza, tunahitaji kujenga na sio kubomoa,” alisema Kiganja.