Duh! Jamaa kumbe wanadai

Friday November 24 2017

 

By YOHANA CHALLE; ARUSHA

WANARIADHA waliokwenda Uganda mapema mwaka huu kushiriki mbio za nyika, wameanza kukidai Chama cha Riadha Tanzania (RT) fedha zao za zawadi.

Katika mashindano hayo ya Dunia ya Nyika yaliyofanyika Machi 26, Tanzania ilishika nafasi ya 13 kwa upande wa wanawake na kuondoka na kitita cha dola 4,000 (Sh8.4 milioni).

Katika fedha hizo, asilimia 60 ilipaswa kugawiwa kwa wanariadha na zilizobaki ni za RT.

Fabian Joseph ambaye alikuwa nahodha wa timu hiyo, amesema hajui lolote kama fedha hizo zimekuja au la, lakini amewasikia wanariadha wenzake wakilalamika juu ya kutopata kifuta jasho hicho kutoka Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF).

“Awali nilisikia fedha hizo zimekuja na baadaye zikarudishwa tena, sikufuatilia sana kwa sababu ni fedha zinazowahusu zaidi waliokuwa wanaunda timu ya wanawake,” alisema Fabian.

Rais wa RT, Anthon Mtaka, alisema wanariadha hao wana haki ya kuuliza juu ya fedha hizo ambazo zilitakiwa kutumwa tangu walipotoka Uganda, lakini haijawa hivyo.

“Kibinadamu wapo sahihi kujua nini kinaendelea kuhusu fedha zile, lakini ukweli ni kwamba bado hazijafika na pindi zitatapotumwa watapewa fedha zao zote. Si Tanzania pekee ambayo haijatumiwa, zipo pia nchi nyingine,” alisema Mtaka.