Ishu nzima ya Ninja, Cannavaro

MASHABIKI wa soka na hasa wale wa Yanga bado walikuwa wakitafakari juu ya kitendo cha aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kuigawa jezi namba 23 kwa beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’, lakini siri yao imevuja.

Cannavaro aliagwa juzi Jumapili katika mchezo maalumu dhidi ya Mawenzi Market uliopigwa Uwanja wa Jamhuri naye kucheza kwa dakika 10 tu na kutoka akikabidhi kitambaa cha unahodha kwa mrithi wake, Kelvin Yondani na kuigawa jezi kwa Ninja.

Hata hivyo, Ninja amefichua sababu ya Cannavaro kuizuia jezi yake namba 23 isistaafishwe kama viongozi walivyotaka na badala yake kuamua kuikabidhi kwake na kuzua maswali mengi kwa mashabiki wa soka nchini wakiwamo wa Yanga.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ninja alisema awali ya yote ameshtushwa na uamuzi wa Cannavaro kumpa heshima kubwa ya kurithi jezi yake, lakini anaamini hiyo imechangiwa na kumuamini tangu akicheza visiwani Zanzibar na ameapa hatamwangusha.

Ninja alisema kupewa jezi hiyo kumemfanya aanze maisha mapya ndani ya Yanga, na ni jambo ambalo linamjengea heshima ndani ya kikosi na hivyo atapambana ili kumuenzi nyota huyo na kuiheshimu jezi hiyo.

“Nilikuwa najichukulia kama mchezaji wa kawaida katika kikosi changu, ila kupitia jezi hii nalazimika kuonyesha utofauti, lengo ni kuendelea kuijengea heshima timu pamoja na jezi hii ambayo imekuwa nuru kwa mashabiki wa Yanga,” alisema.

SAPRAIZI KWAKE

Ninja amesisitiza, Cannavaro kamshtukiza kwa kumpa jezi hiyo kwani hakujua mipango hiyo mapema. Cannavaro ndiye aliyechangia kumvuta Ninja Jangwani akitokea Taifa Jang’ombe ya Zanzibar.

“Haukuwa mpango ulioandaliwa, nimefanyiwa sapraizi, kwani awali nilisikia jezi hiyo inastaafishwa, lakini nikiwa benchi kumpisha mchezaji huyo aweze kucheza dakika chache ili kuwaaga mashabiki na wachezaji, nilishangazwa kwa kuamua kunikabidhi jezi hiyo na kuniambia ananiamini na anaamini nitafanya kitu kikubwa zaidi ya alichokifanya,” alisema Ninja.

Aliongeza baada ya kukabidhiwa alishindwa kuzuia furaha yake na kumwambia anashukuru na kutii heshima aliyompa na alimuahidi kufanya kazi nzuri zaidi kwa lengo la kumuonyesha Cannavaro kuwa hajakosea kumkabidhi jezi.

“Baada ya kunikabidhi aliniambia amenipa ili awe anaiona jezi hiyo ikitumika na anaamini mimi ni mchezaji sahihi hategemei kama nitashindwa kumlindia heshima kama walivyotaka kuilinda viongozi wake waliotaka iwekwe kama kumbukumbu isitumiwe na nyota mwingine yeyote,” alisema.

BABI AMPA TANO

Katika hatua nyingine nyota wa zamani wa kimataifa aliyekuwa nahodha wa Yanga, Abdi Kassim ‘Babi’ amempa tano Cannavaro na kusifu maamuzi yake ya kustaafau akidai ni sahihi japo bado alikuwa na nafasi ya kuendelea kucheza.

Babi alisema wachezaji wanaochipukia katika mchezo huo wanatakiwa kujifunza kupitia kwa mkongwe huyo kutokana na nidhamu, uhamasishaji, uwezo na kudumu kwake katika kikosi kimoja kwa zaidi ya miaka 10.

“Cannavaro ni mtu wa kujitoa, hapendi timu ifungwe, ni mpambanaji nimecheza naye Yanga, timu ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’, ni mchezaji niliyemkabidhi kitambaa cha unahodha katika timu yetu ya taifa nampongeza kwa uamuzi aliouchukua japo ni mapema, ana nafasi ya kuendelea kucheza,” alisema.

“Ukifanya vizuri kwenye timu moja kwa miaka mingi ni vigumu kuonyesha kiwango hicho hicho unapokwenda timu nyingine, hivyo ni vyema kudumu katika kikosi kimoja kwani itakusaidia kukujengea heshima kama alivyofanya,” alisema Babi.