Hawa hapa Mastaa waliokipiga Ligi nyingi kubwa za Ulaya

WAKATI staa wa kimataifa wa Ureno, Cristiano Ronaldo akijiunga na Juventus na hivyo kujikuta akicheza katika Ligi ya tatu kubwa barani Ulaya, kuna wachezaji ambao wanamtazama na kumkebehi kwa jinsi ambavyo wamezurura katika Ligi nne kubwa za Ulaya, England, Hispania, Ujerumani na Italia.

Pepe Reina

Kipa wa zamani wa kimataifa wa Hispania. Alichomoka katika soka la vijana akiwa na Barcelona kabla ya kucheza mechi 30 ndani ya misimu miwili. Alijenga jina zaidi akiwa na klabu ya Villarreal ya hapo hapo kwao Hispania baada ya kutua mwaka 2002.

Mwaka 2005 alinaswa na Liverpool na alicheza kwa mafanikio kwa kipindi cha miaka tisa pale Anfield.

Msimu wa 2013-14 alipelekwa kwa mkopo Napoli ya Italia. Mwaka 2013 alichukuliwa kwa dili la moja kwa moja na Bayern Munich kwa ajili ya kuwa msaidizi wa kipa, Manuel Neuer. Hata hivyo baada ya mwaka mmoja alirudi Italia kukipiga katika klabu yake ya Napoli ambayo ameendelea kuichezea mpaka sasa.

Bojan Krkic

Kinda huyu aliyeibukia Barcelona naye ni mzururaji mzuri wa Ligi kubwa za Ulaya. Kwa sasa yupo kwa mkopo katika kla bu ya Mainz 05 ya Ujerumani baada ya kuchemsha katika klabu ya Stoke City ya England.

Bojan aliibua matumaini makubwa kwa waliokuwa wanamfuatilia wakiamini angefuata nyota za mastaa wakubwa walioibukia katika soka la vijana Barcelona.

Kumbuka kabla ya hajaibukia England tayari alikwenda nchini Italia katika klabu za AS Roma na AC Milan kwa ajili ya kujaribu bahati yake. Ndani ya miaka 26 tu tayari Bojan ameshacheza Ligi ya Hispania, England, Ujerumani na Italia.

Kevin-Prince Boateng

Mmoja kati ya wazururaji wazuri wa Ligi kubwa za Ulaya ni huyu hapa. Staa wa kimataifa wa Ghana ambaye ni mzaliwa wa Ujerumani.

Boateng aliibukia Hertha Berlin na kuonyesha kipaji kikubwa kabla ya kutua Tottenham ya England ambayo hata hivyo alikosa nafasi.

Hata hivyo, baadaye alitua Portsmouth na kuonyesha makali yake.

AC Milan haikujivunga ikamchukua na aliichezea katika vipindi viwili tofauti huku katikati ya vipindi hivyo akikipiga katika klabu ya Schalke.

Baadaye alikwenda Las Palmas ya Hispania na hivyo kucheza La Liga kwa mara ya kwanza. Kwa sasa amerudi kwao Ujerumani kukipiga katika klabu ya Frankfurt.

Obafemi Martins

Mwafrika mwingine aliyepata bahati ya kucheza Ligi nne kubwa za Ulaya ni huyu hapa. Aliibukia kwa kasi Inter Milan mwanzoni mwa miaka ya 2000 kabla ya Newcastle kumsafirisha kwenda England kwa dau la Euro 15 milioni. Alicheza misimu mitatu pale Newcastle huku akifunga mabao 28 katika mechi 88.

Baada ya hapo aliondoka zake na kutua Ligi ya Ujerumani akicheza katika jezi ya Wolfsburg kwa msimu mmoja kabla ya kurudi Ligi Kuu ya England kwa mkopo wa mwaka mmoja klabu ya Birmingham City.

Baadaye akaenda zake Levante ya Hispania kabla ya kutimkia Ligi Kuu ya Marekani kisha China.

Jon Dahl Tomasson

Mmoja kati ya wafungaji wazuri wa mabao kuwahi kutokea katika historia ya Denmark. Mabao yake mengi ya awali aliyafunga katika Ligi Kuu ya Uholanzi akiwa na Heerenveen na kisha baadaye Feyenoord.

Baada ya hapo alianza kuzurura katika klabu mbalimbali za Ligi Kubwa nne za Ulaya Hispania, England, Italia na Ujerumani.

Alianzia Newcastle United ambako hata hivyo mambo hayakwenda sawa. Baadaye aliibukia AC Milan ambako aliibuka kuwa kipenzi cha mashabiki. Alitwaa ubingwa wa Serie A pamoja na taji la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Baadaye aliamua kuionja Ligi Kuu ya Ujerumani Bundesliga kwa kukipiga katika klabu ya Stuttgart lakini mwishowe hakutaka fursa ya kucheza Hispania impite wakati alipotakiwa na Villarreal ya Hispania.

Pierre Wome

Mmoja kati ya walinzi bora wa muda wote nchini Cameroon na Afrika kwa jumla. Katika kipindi cha miaka 16 alichocheza soka la kulipwa barani Ulaya daima alibadili ligi kutoka moja kwenda nyingine.

Alianzia Italia katika klabu ya Bologna lakini mwishowe akajikuta akiwa ameangukia Espanyol ya Hispania. Ndani ya safari yake ya soka aliamua kuionja Ligi Kuu England na kukipiga katika jezi ya Fulham ya London.

Baadaye alirudi nchini Italia ambako alianzia soka la Ulaya kwa kwenda kucheza klabu za Brescia na Inter Milan. Mwaka 2006 aliamua kuionja Ligi Kuu ya Ujerumani kwa kwenda kukipiga Werder Bremen.

Maniche

Mchezaji mwingine aliyezura sana katika soka la Ulaya ni staa huyu wa zamani wa kimataifa wa Ureno. Alijikuta amezigusa Ligi zote kubwa za Ulaya baada ya kuanza maisha yake ya soka Benfica ya kwao Ureno kabla ya kujiunga na Alverca.

Alirudi katika klabu yake ya utotoni mwaka 1999 lakini akauzwa kwenda Porto miaka mitatu iliyofuata na alichukua ubingwa wa Ulaya chini ya Kocha, Jose Mourinho.

Baadaye alikwenda Russia kukipiga Dynamo Moscow msimu wa 2005-06 bila ya mafanikio. Akaenda England kwa mara ya kwanza kucheza kwa mkopo Chelsea chini ya kocha wake wa zamani wa Porto, Mourinho. Hata hivyo hakucheza kwa mafanikio baada ya kujikuta akicheza mechi 11 tu.

Mwishoni mwa msimu aliamua kwenda Hispania kukipiga Atletico Madrid kabla ya kwenda kucheza kwa mkopo kwa kipindi kifupi Inter Milan mwaka 2008.

Mwaka 2009 aliionja Ligi Kuu ya Ujerumani kwa mara ya kwanza baada ya kukipiga na Cologne lakini muda mfupi uliofuata alirudi Ureno kukipiga Sporting Lisbon kabla ya kuamua kustaafu soka mwaka 2011.