Zlatan, Man United wachana kimtindo

Muktasari:

Mshambuliaji huyo msimu huu ameshindwa kucheza mechi nyingi kutokana na kusumbuliwa na majeruhi

MANCHESTER, ENGLAND. Zlatan Ibrahimovic amekamilisha uhamisho wake wa kwenda LA Galaxy akionyesha picha yake pamoja na Simba.

Ibrahimovic  anayejifananisha na Simba alituma video yake akiwa na jezi ya Galaxy: "Los Angeles, karibu Zlatan."

Ibrahimovic na Manchester United wameamua kuchana mkataba uliokuwepo baina yao na staa huyo wa kimataifa wa Sweden jana alitazamiwa kuendelea na maisha mengine kwa kujiunga na klabu ya LA Galaxy.

Dili la Zlatan kwenda Galaxy linatazamiwa kuwa mkataba wa pauni 1 milioni kwa mwaka na lilitazamiwa kutangazwa kama tangazo katika ukurasa mzima wa gazeti maarufu la Marekani, Los Angeles Times na alitazamiwa kwenda California kwa ajili ya kutambulishwa.

Zlatan mwenye umri wa miaka 36 amesaini mkataba mpaka mwishoni mwa msimu na anaweza kucheza mechi yake ya kwanza kwa wababe hao katika pambano la Ligi Kuu ya Marekani dhidi ya watani wao wa jadi LAFC Machi 31.

United ilithibitisha jana kwamba walikuwa wameukomesha mkataba wa staa huyo ambaye kwa mara ya kwanza sasa atacheza nje ya bara la Ulaya baada ya kutamba katika klabu za Barcelona, Ajax, Paris Saint-Germain, Juventus, Inter Milan na AC Milan.

Zlatan mwenyewe aliandika katika mtandao wake akisema “Mambo mazuri ufika mwisho na huu ni wakati wa kuendelea na maisha mengine baada ya kuwa na misimu mizuri miwili na Manchester United.”

“Asante sana kwa klabu, mashabiki, timu, kocha na wafanyakazi wengine ambao walishirkiana na mimi katika sehemu hii ya historia yangu.:”

Zlatan alikuwa akihusishwa kwa muda mrefu kujiunga na klabu hiyo ambayo iliwahi kuwachukua David Beckham na Steven Gerrard katika nyakati mbalimbali na sasa Zlatan anakwenda kufungua ukurasa mpya klabuni hapo.