Zawadi za Sofapaka zaamsha morali kwa wachezaji

Monday September 11 2017

 

By Na THOMAS MATIKO

Kocha Sam Ssimbwa wa Sofapaka FC,  iliyokoswakoswa kushuka daraja msimu uliopita, amesema mpango waliouanzisha uongozi wa klabu kuwatuza wachezaji wake watatu bora kila mwezi,  ndio umewafanya moto wa kuotea mbali msimu huu.

 Tangu Agosti mwaka  huu, baada ya uongozi kutangaza mpango huo, Sofapaka ilichupa kutoka nafasi ya tano hadi ya pili ambayo imeganda mpaka sasa ikiwa nyuma ya Gor wenye pointi 47 kwa alama sita.

 Wikendi hii, Sofapaka iliendeleza  makali yake kwa kuilima Chemelil Sugar 4-1 iliyofuatiwa na sare 1-1 dhidi ya Posta Rangers. Kabla ya hapo Batoto Ba Mungu waliwalima Nzoia Sugar 3-1 na Nakumatt 5-2.

 Kwenye tuzo hizo za Sofapaka, mchezaji bora  wa mwezi hulambishwa Ksh30,000, nambari mbili Ksh20,000 huku mfungaji bora wa mwezi akila Ksh30,000.