Zamalek waje tu

Muktasari:

Droo ya mechi za awali kuwania kutinga katika makundi ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu Afrika, itafanyika kesho jijini Cairo, Misri na ndipo timu hizo zitajua zitaanza na nani.

KESHO Jumatano kabla ya swala ya Magharibi, tayari wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya kimataifa, Yanga itakayocheza Ligi ya Mabingwa Afrika na Simba itakayokipiga Kombe la Shirikisho Afrika, zitakuwa zimeshawafahamu wapinzani wao.

Droo ya mechi za awali kuwania kutinga katika makundi ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu Afrika, itafanyika kesho jijini Cairo, Misri na ndipo timu hizo zitajua zitaanza na nani.

Lakini hata kabla ya droo hiyo haijafanyika, makocha wa klabu hizo na hata wawakilishi wa Zanzibar, JKU na Zimamoto, tayari wameshachungulia orodha ya timu pinzani zilizopo kwenye michuano hiyo.

Baada ya kuangalia orodha hiyo, mabenchi ya ufundi ya timu hizo yametamka tamko ambalo linaoonyesha kuwa mwakani timu yoyote itakayotia mguu kuvaana na klabu za Tanzania, lazima iwe imejipanga la sivyo itaaibika.

Kocha Msaidizi wa Simba, Masudi Djuma, ameshtuka mapema na kuamua kuwapa vijana wake stamina kwa kuwapigisha tizi la nguvu ufukweni, huku akitamka kwamba iwe Enyimba ya Nigeria, Nkana Rangers au Green Buffaloes za Zambia na hata Waarabu wao waje tu, lakini ni lazima wapigwe safari hii.

Mara ya mwisho Simba kushiriki michuano ya Afrika ilikuwa mwaka 2013 ilipocheza Ligi ya Mabingwa na kutolewa kwa aibu katika raundi ya awali kwa kipigo cha mabao 5-0 toka kwa Recreativo de Libolo ya Angola.

Hata hivyo, Djuma alisema hana hofu ya klabu watakayopangwa nayo hiyo kesho kwa sababu anakiamini kikosi chake na mipango inaendelea ili kujiweka vizuri zaidi.

Wachezaji wa Simba jana Jumatatu walipiga tizi la maana ufukweni Coco na leo Jumanne wataingia Gym ya Chuo cha Polisi Kurasini ili kuzidi kujiweka fiti kabla ya kusikilizia kesho watavaana na timu ipi katika michuano ya CAF-shirikisho la soka la Afrika.

Kocha Djuma alisema wanatambua wanaweza kupangwa na ama Enyimba, Zamalek, Raja Casablanca, Club Africain ama USM Alger au Al Ahly Shendi, lakini kwao ni freshi tu.

“Usajili tulioufanya dirisha kubwa na unaoendelea kwenye dirisha dogo unatupa matumaini ya kukabiliana na klabu yoyote ya Afrika, hatujali itatoka Nigeria, Zambia, Ivory Coast, Afrika Kusini ama Afrika Kaskazini,” alisema kocha huyo Mrundi akiungwa mkono na Nahodha Msaidizi John Bocco ‘Adebayor’.

“Nitakaa chini na kocha Mkuu (Joseph Omog) akirudi ili kuangalia sehemu gani ya kwenda kuweka kambi kwa ajili ya maandalizi itakayotupa umakini mkubwa kuelekea kwenye michuano hiyo kama ilivyokuwa maandalizi ya Ligi Kuu Bara,” aliongeza.

“Kuhusu kambi ya michuano ya kimataifa itategemea na timu tutakayopangwa kuanza nayo, ila itakuwa ya aina yake kwa sababu tuna kikosi kizuri na fedha pia zipo za kufanya lolote mradi tupate mafanikio.”

Naye Meneja wa Simba, Richard Robert, alisema baada ya ratiba kutoka na kujijua wapo katika kundi lenye timu kutoka nchi gani, watakaa kikao na makocha kupendekeza sehemu gani wakajichimbie mapema.

Mechi za awali za michuano hiyo zitapigwa kati ya Febrauri 9-18 kwa mechi za awali na marudiano na zitakazofuzu zitatinga raundi ya kwanza ambazo mechi zake zitachezwa kati ya Machi 9-18.

HATA YANGA FRESH

Kocha wa Yanga, George Lwandamina, alishasisitiza kuwa maadamu wao ni mabingwa wa nchi na wataiwakilisha nchi, hawana presha na timu ya kukutana nayo ilimradi mabosi wake watenge mzigo wa maana kwa maandalizi yao.

Mzambia huyo anaamini vijana wake hawatamuangusha na kwamba tayari wameshajua tatizo lililowaangusha msimu uliopita waliposhindwa kuingia makundi baada ya kutolewa raundi ya kwanza na Zanaco kwa faida ya bao la ugenini baada ya Yanga kulazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani kabla ya suluhu ugenini nchini Zambia.

OMOG, OKWI HAOOO

Katika hatua nyingine Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog na nyota wote wa kigeni waliokuwa mapumzikoni makwao, wanatarajia kurejea nchini keshokutwa Alhamisi.

Nyota hao wa kigeni ni kinara wa mabao wa Ligi Kuu, Emmaneul Okwi, James Kotei, Method Mwanjali, Haruna Niyonzima, Nicholas Gyan, Laudit Mavugo na Juuko Murshid. Wachezaji hao na kocha Omog walipewa siku 14 za mapumziko.

Vigogo Ligi ya Mabingwa:

Al Ahly, Esperance, Etoile du Sahel, TP Mazembe, AS Vita, ES Setif, MC Alger, Mamelodi Sundowns, Wydad Casablanca, Asec Memosas, Zanaco na Zesco.

Vigogo Kombe la Shirikisho:

Zamalek, Enyimba, Raja Casablanca, DC Motema Pembe, USM Alger, Nkana Rangers, SuperSporr United na CR Belouizdad.