VIDEO: Zahera awatega Tambwe, Makambo

KIKOSI cha Yanga leo jioni kitashuka kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini hapa ili kuivaa na Mawenzi Market katika mechi maalumu ya kumuaga aliyekuwa nahodha wa zamani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, huku Kocha Mwinyi Zahera akiwatega kimtindo nyota wake wanne, akiwamo Amissi Tambwe na Heritier Makambo.

Kocha huyo kutoka DR Congo amewapa mtihani mzito nyota hao wanaocheza nafasi ya mbele kwa kuhakikisha wanafunga mabao mengi ili kulinda ajira zao Jangwani kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara itakayoanza siku 10 zijazo.

Kocha huyo amewapangia kila mshambuliaji wa timu hiyo idadi ya mabao ambayo wanatakiwa kuyafunga katika ligi ijayo, huku Tambwe na Makambo wakipewa mtihani mzito zaidi kuliko wenzao watatu.

Heritier Makambo- 15

Zahera ameanza na washambuliaji wake wawili wa kati wa kwanza ni Mkongomani mwenzake, Heritier Makambo amemwambia kwa msimu mmoja anatakiwa kufunga sio chini ya mabao 15 ili awe salama.

Kocha Zahera alisema anamjua Makambo na kwamba kazi hiyo sio ngumu kwake kutokana na ujuzi alionao wa kufunga mabao akitakiwa kutekeleza hilo ndani ya msimu mmoja.

Amissi Tambwe-15

Kutoka kwa Makambo akamgeukia Amissi Tambwe akisisitiza kwanza Mrundi huyo na Makambo hawataweza kucheza pamoja badala yake watakuwa wanapishana na kwamba naye anatakiwa kufunga idadi ya mabao kama ile ya Makambo.

Kocha huyo alisema Tambwe bado ni mshambulaji bora na kwamba kikosi chake kitategemea ujuzi wake wa kufunga lakini ameshamwambia anataka ajitume zaidi kuweza kufikia malengo hayo.

Kwa misimu miwili na nusu tu, ukiondoa msimu uliopita aliyoichezea Yanga, Tambwe amekuwa kinara wa mabao akifunga jumla ya mabao 45. Iwapo atakuwa fiti idadi hiyo inaweza kuwa nyepesi kwa Mrundi huyo ambaye msimu uliopita hakufunga hata bao moja kutokana na kuwa majeruhi kwa msimu mzima.

Ngassa na Kaseke-8

Alipotoka hapo akawageukia viungo washambuliaji wa pembeni akianza na Deus Kaseke akasema kwa kuwa jukumu lao kubwa litakuwaa kuwatengenezea nafasi washambuliaji wa kati, lakini naye anatakiwa kufunga sio chini ya mabao saba mpaka nane au zaidi.

Idadi kama hiyo pia alimpa winga mkongwe Mrisho Ngassa ambapo naye akampa jukumu kama hilo akitakiwa kufunga mabao hayo saa mpaka nane au zaidi akiridhika na kasi ya mkongwe huyo.

Msikie Zahera

Kocha zahera alisema idadi hiyo kama itafikiwa ina maana wachezaji hao wanne watakuwa wameweza kufikisha mabao 46 katika kimo cha chini.

“Nataka kuona washambuliaji wa kati wanakuwa na uwezo wa kufunga sina tatizo nao Makambo namjua vyema hiyo idadi ya mabao haiwezi kuwa shida kwake anatakiwa kujituma na kutuliza akili uwanjani,” alisema Zahera.

“Hata Tambwe nimeangalia rekodi zake anaweza kufunga tutatengeneza timu itakayoweza kuzalisha mabao mengi lakini hawa wawili Makambo na Tambwe watakuwa wakipishana hawataweza kucheza pamoja.

“Hao kina Kaseke na Ngassa nao wanatakiwa kuhakikisha kwanza wanawatengenezea nafasi washambuliaji wa kati lakini nao kila mmoja anatakiwa kufikisha mabao saba, nane au zaidi. Kinachotakiwa ni mabao, huwezi kusema unafanya vizuri kama hufungi. ”