Zahera atoa onyo kwa Stand United

Muktasari:

Upande wa mabeki alionekana kuwafundisha namna ya kukaba na kuzuia mshambuliaji ambayo yanaelekezwa langoni kwao

Dar es Salaam.WAKATI Stand United inatamba kuishushia kipigo Yanga kupitia straika wake Mrundi, Bigirimana Blaise, Kocha wa mabingwa hao wa zamani, Mwinyi Zahera ameonya kuwa ameandaa jeshi la maangamizi na suala la ushindi halina mjadala.
Zahera, ametumia zaidi ya saa mbili kuwanoa nyota wake Herietie Makambo, Ibrahim Ajibu, Mrisho Ngassa, Deus Kaseke na Pius Buswita kuwafundisha namna ya kupiga mashuti ya mbali yenye kuleta matokeo mazuri.
Upande wa mabeki alionekana kuwafundisha namna ya kukaba na kuzuia mshambuliaji ambayo yanaelekezwa langoni kwao.
Zahera alitumia pia saa nne kukinoa kikosi hicho kabla ya kuwagawa wachezaji katika makundi ambapo aliwatenga mabeki, washambuliaji na viungo.
"Tunahitaji kupata mabao mengi katika mechi dhidi ya Stand United ili tukae kwenye nafasi nzuri katika msimamo.
"Stand United ni timu nzuri nimefuatilia baadhi ya mechi zao za nyuma hivyo, tunajipanga kwa ushindani ili kutimiza malengo yetu," alisema Zahera.
Yanga ikiwa na matumaini ya ushindi, Stand United wametamka kuwa wanakuja na mtu anaitwa Blaise hivyo wajiande kwa kipigo.
Kocha Msaidizi wa Stand United, Athuman Bilali 'Bilo' alisema anawashangaa Yanga kutamba na Makambo wakati kiwango chake ni cha kawaida.
"Makambo ni nani? anaweza kuuzidi uwezo wa Blaise! Wawaulize Simba wataambiwa habari yake, tunaingia kesho (leo) tukiwa na jeshi kamili la kuchukua pointi tatu mbele ya mashabiki wao," alisema Bilo.