Zahera alipangua jeshi lake Stand

Muktasari:

Msimu uliopita Stand haikuvuna chochote kwa Yanga kwani ilipigwa nje ndani kuanzia kule kwao Shinyanga na Dar, hivyo wanaporudi leo Taifa akili yao ni kutaka kuwazuia wenyeji wao na kusaka pointi tatu.

BENCHI la Ufundi la Yanga linafahamu kiu ya mashabiki wake katika mechi za Ligi Kuu Bara na leo Jumapili kikosi chao kitashuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku Kocha Mwinyi Zahera akipangua kidogo jeshi lake dhidi ya Stand United.

Msimu uliopita Stand haikuvuna chochote kwa Yanga kwani ilipigwa nje ndani kuanzia kule kwao Shinyanga na Dar, hivyo wanaporudi leo Taifa akili yao ni kutaka kuwazuia wenyeji wao na kusaka pointi tatu.

Hata hivyo, Kocha Zahera amewashtukia wageni wao mapema na kujipanga ili kupata ushindi, huku akilipanga jeshi lake kucheza soka la kushambulia kwa mashambulizi makali na kama Stand haitajipanga basi itamaliza wikiendi vibaya.

Kocha huyo kwanza amepangua kimtindo kikosi chake katika safu yake ya ulinzi amemjumuisha kijana mmoja mdogo mwenye kasi, Paul Godfrey ‘Boxer’ aliyepewa jina hilo la pikipiki ili kuziba nafasi ya nahodha msaidizi Juma Abdul.

Abdul aliumia katika mchezo wa kwanza wa ligi bado hajawa fiti na kuziba nafasi yake Zahera akampa nafasi kinda huyo ambaye katika mazoezi ya timu hiyo kazi yake sio mchezo.

Kinda huyo huenda ataanza sambamba na kipa Benno Kakolanya, Gadiel Michael kushoto wakati mabeki wa kati wakiwa Andrew Vincent ‘Dante na nahodha mkuu Kelvin Yondani.

Zahera anaweza asifanye mabadiliko katika kiungo chake kwani jana alionekana akikomaa na Papy Tshishimbi, Feisal Salum, Mrisho Ngassa na Deus Kaseke ambao wanaweza kuwa wanabadilisha kimtindo mifumo miwili. Uwepo wa viungo hao Yanga inaweza kutumia mifumo ya 4-3-3 au hata 4-4-2 kulingana na Stand watakavyokuja katika mchezo huo.

Mabadiliko mengine ni pale mbele Zahera ameonekana jana katika mazoezi akimjaribu Ibrahim Ajib kucheza sambamba na Heritier Makambo. Ajib hakuanza katika mchezo wa kwanza na alitokea benchi na kurudi kwake kunamfanya Matheo Antony kurejea benchi.

Mazozi ya mwisho jana pale Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini Zahera alionekana kuhimiza mashambulizi ya haraka akitaka pasi za haraka zipigwe kufika golini na wakifika hapo hakuna kuremba ni kutafuta mabao.

Hata hivyo, Yanga yenye pointi inatakiwa kuwa makini na Stand hasa straika wao Mrundi Bigirimana Braise mwenye nguvu na akili ya kufunga ambaye kasi yake imeifanya klabu yake kuvuna pointi sita.

Zahera, alisema amewaanda vijana wake kusaka alama nyingine tatu baada ya zile za Mtibwa Sugar katika mechi yao ya awali, huku Kocha Msaidizi wa Stand Athuman, Bilal ‘Bilo’ akisisitiza wamekuja Dar kusaka pointi tatu, japo anakiri mechi itakuwa ngumu.

“Tumejiandaa kwa ajili ya kuvuna pointi tatu, hatuidharau Yanga, lakini wasitarajie mteremko kwetu, lengo letu kuendelea kujiweka pazuri kwenye msimamo mechi za mapema, ili tusihenyeke mwishoni,” alisema Bilo. Mbali na mechi hiyo ya Dar, kule Mbeya wanaoburuza mkia Mbeya City watakuwa wenyeji wao Alliance FC ya Mwanza kwenye Uwanja wa Sokoine.

KABWILI ATIMULIWA

Katika hatua nyingine, wakati baadhi ya mashabiki wao bado hawajakunjua nafsi juu ya kitendo cha baadhi ya wachezaji wao kutimuliwa na Kocha Mkuu wa Taifa Stars Emmanuel Amunike wakiona wamebaguliwa, huku Yanga walifurahia hilo. Hata hivyo kibao pale Jangwani kimebadilika baada ya Kocha Mwinyi Zahera kuanza kutumia falsafa ya aina hiyo kwa kumtimua kambini kipa chipukizi, Ramadhani Kabwili kwa kuchelewa muda wa kupiga msosi. Inaelezwa Zahera hakufurahishwa na kiungo wake, Feisal Salum kuwa kati ya nyota waliotimuliwa na Amunike na kuanza kujenga nidhamu ya muda kambini na Kabwili akawa wa kwanza kunaswa na hatua ya kocha.

Zahera aliwaita wachezaji wake siku nne zilizopita akiwaambia kwamba siku hiyo jioni wataingia kambini kujiandaa na mchezo dhidi ya Stand United.

Hakuishia hapo akawaambia kila mchezaji anaweza kuja muda anaoutaka katika hoteli watakayoitumia lakini muda wa chakula cha jioni kila mchezaji anatakiwa kuwa ndani ya bwalo la chakula bila kuchelewa.

Wachezaji wote wakatekeleza lakini walipofika ndani ya bwalo hilo Zahera akahoji wasaidizi wake anayejua alipo Kabwili.

Hakukuwa na mwenye taarifa zake na Mkongomani huyo akampigia na kumwambia: ‘Kama uko njiani au nyumbani basi geuze, utarudi baada ya mechi na uje na maelezo.”

Hatua hiyo iliwashtua mastaa wa Yanha na kila mmoja alionekana kuanza kumwogopa kocha huyo.