Z’Bar pigeni haoo mbebe ndoo

Muktasari:

  • Timu ya Zanzibar Heroes inatarajiwa kushuka Uwanja wa Kenyatta kuvaana na wenyeji Kenya huku Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla wakiiombea dua njema ili kurejea visiwani wakiwa na taji hilo.

KABLA swala ya Magharibi haijaswaliwa, itakuwa imefahamika nani amekuwa bingwa mpya wa michuano ya Chalenji inayofikia tamati leo mjini Machakos, Kenya, lakini gumzo kubwa visiwani hapa ni mafanikio ya mashujaa wa Zenji.

Timu ya Zanzibar Heroes inatarajiwa kushuka Uwanja wa Kenyatta kuvaana na wenyeji Kenya huku Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla wakiiombea dua njema ili kurejea visiwani wakiwa na taji hilo.

Zanzibar waliivua ubingwa Uganda juzi Ijumaa kwa kuilaza kwa mabao 2-1 katika mechi ya nusu fainali ya pili baada ya ile ya awali wenyeji Kenya kuing’oa Burundi kwa bao 1-0 lililopatikana ndani ya muda wa nyongeza. Ushindi wa Zanzibar dhidi ya Uganda na kuelekea katika mechi yao ya leo imewafanya Wazanzibar kujivunia timu hiyo, huku serikali ikisema haina mpango wa kuleta kocha wa kigeni kwa vile waliopo wapo vizuri kinoma.

Naibu Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Choum Kombo Khamis alisema hayo wakati akizungumzia mwenendo wa timu hiyo mjini hapa jana.

Alisema Zanzibar imejaaliwa kuwa na vipaji vingi vya ufundishaji hivyo, hawaoni sababu ya kuharibu fedha kutafuta kocha kutoka nje ya nchi, huku Zanzibar kila uchao ikizalisha watalaam wa soka.

Alitolea mfano kocha Morocco kwa kusema kuwa ana uwezo mkubwa wa kufundisha soka ndio maana hadi wakati huu anaendelea kuiletea sifa Zanzibar kupitia kikosi cha Heroes anachokiongoza katika mashindano ya Chalenji.

Makamu wa Rais wa SMZ, Balozi Seif Ali Iddi alisema hatua iliyofikia Heroes ni adimu kufikia katika kipindi kirefu cha ushiriki wa mashindano hayo na anaamini watarejea na ubingwa katika mechi yao ya fainali ya leo.

“Ukweli kuwa hatua iliyofikia timu yetu imetutangaza nje ya nchi, nasi tutaongeza nguvu zetu kuiunga mkono,” alisema.

Zanzibar imeweza kutwaa ubingwa wa Chalenji mara moja tu mwaka 1995 kitu ambacho nyota wake wameahidi kukifanya kule Kenya leo.