Yanga yawatuliza Ngoma, Tambwe yampa mkono wa kwa kheri Bossou

Muktasari:

Tambwe amerejea nchini akitokea Burundi alipokuwa kwa mapumziko na kukutana na viongozi wa Yanga makao makuu ya klabu hiyo Jangwani, Dar es Salaam huku Ngoma akitarajiwa kutua leo Jumanne akitokea Zimbabwe.

 Uongozi wa Yanga umesema washambuliaji wake Donald Ngoma na Amiss Tambwe wataendelea kuichezea timu hiyo msimu ujao.

Tambwe amerejea nchini akitokea Burundi alipokuwa kwa mapumziko na kukutana na viongozi wa Yanga makao makuu ya klabu hiyo Jangwani, Dar es Salaam huku Ngoma akitarajiwa kutua leo Jumanne akitokea Zimbabwe.

Ngoma alikuwa akihusishwa kujiunga na Simba, lakini katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa amelithibitishia kuwa Ngoma ataendelea kuitumikia timu hiyo.

"Ngoma ni mchezaji wa Yanga hadi Julai atakapomaliza mkataba, pia tumeshazungumza naye na tumekubaliana atabaki Yanga na yuko kwenye programu za kocha msimu ujao," alisema Mkwasa.

Mkwasa alisisitiza hadi sasa klabu yake imekamilisha usajili wa wachezaji watatu wa kigeni.

"Tunao wachezaji watatu wa kigeni ambao tumewasajili kipindi hiki," alisema Mkwasa huku akigoma kuwataja majina kwa madai kwamba wamewaandalia utaratibu maalumu wa kuwatambulisha.

Mkwasa alifafanua hatma ya beki Vicent Bossou kwamba Yanga imelazimika kumpa mkono wa kwaheri baada ya kushindana naye.

"Bossou hatokuwepo, Yanga ilipenda kuendelea naye, lakini tatizo ni mchezaji mwenyewe amekataa kuongeza mkataba.".

Mbali na Bossou, tayari Yanga imeachana na kiungo wake Mnyarwanda, Haruna Niyonzima pia kuna tetesi kuwa kiungo Justin Zullu 'Mkata Umeme' uenda akaondoka klabuni hapo.