Yanga yapigwa, Simba kuivaa Mtibwa Kesho

Saturday August 12 2017

 

By Oliver Albert,Mwananchi oalbert@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Bao la kujifunga la beki wa kati Abdallah Shaibu'Ninja' limeizamisha Yanga kwa bao 1-0 mbele ya Ruvu Shooting katika mchezo mkali wa kirafiki uliofanyika leo jioni kwenye Uwanja wa Chamazi Complex, Chamazi.

Shaibu alikuwa akijaribu kuokoa kwa kichwa krosi ya iliyopigwa na Shalla Juma wa Ruvu Shooting na mpira kwenda moja kwa moja wavuni.

Huo ni mchezo wa pili wa kirafiki kwa Yanga baada ya ule dhidi ya Singida United ambao mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara waliibuka na ushindi wa mabao 3-2.

Yanga itaondoka kesho asubuhi kwenda Zanzibar na usiku itacheza mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya Mlandege kwenye Uwanja wa Aman visiwani humo.

Timu hiyo Jumatatu itatimkia Pemba kuweka kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba utakaofanyika Agosti 23.

Wakati huo huo, kesho Jumapili, Simba itaivaa Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa kirafiki utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Huo unakuwa mchezo wa pili kwa Simba tangu itoke Afrika Kusini ilikoweka kambi ya wiki tatu. Mchezo wa kwanza wa kirafiki iliifunga Rayon Sport ya Rwanda bao 1-0 katika Tamasha la Simba Day.

Baada ya mchezo huo, Jumatatu Simba itakwenda kuweka kambi ya wiki moja Zanzibar kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga utakaofanyika Agosti 23.