Yanga yapewa Rayon, Gor Mahia, Alger

Muktasari:

Yanga mara mbili katika hatua ya makundi wamemaliza wakiwa wa mwisho

Dar es Salaam. Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga imepangwa Kundi D pamoja na  Gor Mahia ya Kenya, Rayon Sport ya Rwanda na USM Alger ya Algeria katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika droo iliyopangwa leo makao makuu ya CAF, Cairo, Misri imeshudia kwa mara ya kwanza Afrika Mashariki ikiwa na timu tatu na zote zimepangwa katika kundi mmoja pamoja na miamba ya Algeria.

Yanga kupangwa kundi hilo imetoa mwanya kwao iwapo watajipanga vizuri wanaweza kufuzu kwa robo fainali na hata kutinga fainali na kuweka historia mpya katika mashindano hayo.

Katika kundi A zimepangwa timu za Asec Mimosas ya Ivory Coast, Raja Club Athletic ya Morocco, As Vita ya DR Congo na Aduana Stars FC  ya Ghana.

Kundi B lina timu za RS Berkane ya Morocco, El Masry ya Misri, UD Songo (Msumbiji) na Al Hilal ya Sudan.

Katika kundi C  lina timu za Enyimba FC ya Nigeria, Williams Ville ya Ivory Coast, CARA Brazaville ya Congo na Djoliba AC ya Mali.

Kila timu kwenye kundi itacheza mechi 6 ikiwa mechi 3 nyumbani na mechi 3 ugenini.

Mechi ya Yanga itachezwa kati ya Mei 4-6, wakati mechi ya itachezwa Mei 15-16, kabla ya mapumziko ya kupisha Kombe la Dunia na mashindano hayo yataendelea tena Julai 27-29 na Agosti 17-19 na mechi ya makundi ya mwisho itachezwa Agosti 28-29.

Baada ya mechi za makundi kuisha droo ya robo fainali  na nusu fainali ya Kombe la Shirikisho itapangwa Septemba 03.

Mechi ya kwanza ya robo fainali itachezwa Septemba 14-16 huku zile za marudiano ni September 21-23, wakati mechi za nusu fainali ya kwanza itachezwa Oktoba 2-3 na ile za marudiano ni Oktoba 23-24 wakati fainali itachezwa  Novemba 23-25, na marudiano itachezwa Novemba 30 au Desemba 02.

Ratiba

Mei 6: USM Alger  v Yanga

Mei 16: Yanga v Rayon

Julai 18: Gor Mahia v Yanga

Julai 29: Yanga v Gor Mahia

Agosti 19: Yanga v USM Alger

Agosti 29: Rayon v Yanga