Yanga yamsapraizi Cannavaro

YANGA bado inaendelea kumfanya sapraizi nahodha wao wa zamani, Nadir Haroub 'Cannavaro'kwani baada ya kumpandisha cheo na kuwa Meneja mara baada ya kustaafu kucheza soka, sasa wameamua kuistaafisha namba yake ya jezi.

Mabosi wa Yanga wamesema namba 23 aliyokuwa akiitumia beki huyo wa kati wataistaafisha na kutuzwa kama heshima na kumbukumbu maalumu ya kile alichoifanyia klabu hiyo aliyoichezea kwa mafanikio makubwa.

Ipo hivi. Mabosi wa Yanga walitangaza kumstaafisha Cannavaro na sasa ni meneja wa timu na pia wamemuandalia mechi ya kumuaga itakayopigwa Agosti 12, lakini wakaona haitoshi na kuamua kuitaifisha namba aliyokuwa akiitumia Jangwani.

Habari kutoka ndani ya Yanga kwa mmoja wa viongozi wa timu hiyo, zilisema wameamua kuistafisha na jezi yake, akidai wanahofia anaweza akavaa mchezaji ambaye hatafiti kazi zake.

"Cannavaro alikuwa mchezaji kiongozi ndani na nje ya uwanja ameifanyia mambo makubwa Yanga hakuna asiyetambua mchango wake nadhani kufanya hivi kutatoa changamoto kwa wachezaji wanaochipukia na waliopo katika timu mbalimbali." kiongozi huyo aliyeomba kuhifadhiwa jina alisema.

Katika hjatua nyinginenyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Ally Mayay aliupongeza uongozi wa timu hiyo kwa kuthamini mchango wa Cannavaro na kuweka wazi wamefanya kitu kizuri sana kulingana na mchango wa mchezaji huyo.

Mayay aliye pia mchambuzi maarufu wa soka nchini, alisema Cannavaro ameiongoza Yanga katika nyakati zote hivyo kumfanyia ivyo ni kutoa funzo kwa wengine kuiga mazuri aliyoyafanya ili na waweze kupewa heshima na timu zao.

"Sio kitu kigeni kilishafanywa na timu nyingi kubwa mfano ni vilabu mbalimbali vimeshastafisha jezi za nyota wao kwa sababu tofauti tofauti. Manchester City walistaafisha jezi namba 23 ya Marc-Vivien Foe baada ya nyota huyo wa Cameroon kufariki uwanjani, Napoli pia walistaafisha jezi namba 10 ya Diego Maradona, Inter Milan jezi namba 4 ya Javier Zaneti na klabu nyingine nyingi," alisema.

Alisema Cannavaro alikuwa nahodha wa Yanga kwa muda mrefu tangu alipostaafu Shadrack Nsajigwa na kumwachia kitambaa naye anakiachia rasmi Agosti 12.

Naye straika wa zamani wa kimataifa aliyetemba na klabu za Tumbaku Morogoro, Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella alisema Yanga haijamtendea haki Cannavaro kwa kumuandalia timu ndogo ili kumuaga kwa heshima.

"Nimesikia wanacheza na timu inayoshiriki Ligi Daraja la kwanza sijapendezwa na hilo kwanza walitakiwa kumtafutia timu kubwa kwa sasa naona kama maigizo na kuhusiana na suala la kustaafisha jezi ya mkongwe huyo pia naona kama wanaiga tu kwasababu kwa upande wewtu bado hatujafikia huko," alisema Mogella.