Yanga yamnasa feisal kimafia

Muktasari:

  • Jana asubuhi Yanga walipata taarifa kuwa, watani wao Simba tangu usiku wa juzi walimbeba kiungo Mzenji, Fesail Salum ‘Totoo’ kwa nia ya kumalizana naye jana katika usajili wa kushtukiza na fasta wakafanya akili moja matata.

ILIKUWA kama filamu flani hivi la kibabe. Ndio, mabosi wa Yanga wamepindua meza hii unaweza kuiita kitemi baada ya kuchukua viungo wawili, huku mmoja akimchomoa mmoja mikononi mwa matajiri wa Simba waliomteka juzi usiku ili wamsainishe fasta.

Iko hivi. Jana asubuhi Yanga walipata taarifa kuwa, watani wao Simba tangu usiku wa juzi walimbeba kiungo Mzenji, Fesail Salum ‘Totoo’ kwa nia ya kumalizana naye jana katika usajili wa kushtukiza na fasta wakafanya akili moja matata.

Akili ya Simba kumkubali Feisal ni kutokana na mechi ya juzi ya nusu fainali ya Kombe la Kagame waliopata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKU na kiungo huyo kupiga mpira mwingi kinoma.

Usiku huohuo Simba hawakulaza damu wakambeba Feisal hadi katika mjengo wa bosi mmoja wa usajili wa Simba, kisha wakampa ofa iliyomtoa macho lakini kiungo huyo akawaambia anahitaji muda afikirie.

Simba hawakutaka kiungo huyo aondoke hivyohivyo bila kusaini wakamtisha zaidi kwa kumpeleka mpaka kwa Bilionea wao Mohamed Dewji ‘MO’ ili aweke msukumo lakini kijana akasema: “Jamani nimekubali lakini haya mamilioni na gari mnavyotaka kunipa nipeni muda nifikirie kesho (jana) tuonane,” anasimulia Feisal.

YANGA WASHTUKA

Mabosi wa Kamati ya Usajili ya Yanga wakasikia taarifa hiyo haraka wakajikusanya na kutaka kubadili upepo na walichofanya wakawawahi watani wao kwa kutinga hoteli waliyofikia JKU saa moja kabla ya muda Simba waliopanga kumchukua Totoo.

Yanga ikiongozwa na Mwenyekiti wake wa Usajili, Hussein Nyika, Makamu wake Mustapha Ulungo na Mjumbe wao, Lucas Mashauri wakaingia vitani kwa kutuma vijana wao watatu wakiwa ndani ya Noah ambao sio tu Feisal wakawasomba mpaka viongozi wa JKU ili kila kitu kimalizwe.

Taarifa ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba Yanga ilishatangulia kumsainisha mkataba wa awali Feisal mapema wakati wa Kombe la Mapinduzi lakini hawakumalizana

SINGIDA NAKO

Baada ya Yanga kumuwahi Feisal, Singida nao wakaingia vitani na kwenda kumsainisha mkataba kama huo lakini nao wakabakiza hatua moja kumalizana na klabu yake.

Wakati jana picha za Feisal zikivuja kwamba amesaini Singida, Mwanaspoti linafahamu kwamba Yanga ilishazungumza na mmoja wa wamiliki wa timu hiyo ya Singida aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba ambaye mdau mkubwa wa Yanga alikubaliana na Yanga kuwaachia Feisal, akiwataka kumalizana naye kwa kumpa fedha zake pamoja na kumalizana na klabu yake.

YANGA v FEISAL TMK

Jana asubuhi baada ya Yanga kumteka Feisal kwa Noah walimshusha maeneo ya Temeke walipokubaliana kila kitu huku kiungo huyo akifichua mbele ya viongozi wa JKU kuwa Singida kupitia Mwigulu wamemruhusu atue Yanga kiulaini.

Kilichofuata baada ya hapo kiungo huyo alikubali kutoka Singida kisha kutakiwa kusaini mkataba mama wa Yanga tayari kwa kutua kwa wawakilishi hao wa Kombe la Shirikisho msimu huu. Baada ya kauli hiyo ya Feisal iliwavunja moyo viongozi wa JKU kisha kuwataka Yanga kumalizana na klabu yao ambapo waliingia makubaliano ya kumalizana ili kiungo huyo asaini.

SIMU ZA SIMBA

Wakati wote wa kikao hicho Simba ilikuwa haijakata tamaa walikuwa bado wanapiga simu kwa viongozi wa JKU na hata ile ya Feisal wakitaka achomoke ili asaini mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Sh35 milioni, mshahara wa 2 milioni na gari safi. Kuona hivyo, Yanga ikahamisha kikao chake mpaka katikati ya jiji majira ya mchana huku wakimtaka kiungo huyo kuzima simu zake zote ili mazungumzo yao yakamilike zoezi ambalo lilikamilika majira ya saa 9:30 alasiri.

ATUA KUSAINI

Baada ya mazungumzo hayo Feisal alitua Jangwani saa 10:25 jioni tayari kwa kupewa mkataba na kusaini akisubiri kila kitu kimalizwe na uongozi wa JKU na Yanga zoezi ambalo lilikamilika na kuwafanya mashabiki wa Yanga waliokuwa wanapiga stori kujiuliza wanasajiliwa kina nani kulipuka kwa furaha baada ya kumuona kiungo huyo.

Wakati Feisal akimaliza kusaini, tayari Yanga ilishamuweka sawa kiungo mwingine Jafary Mohamed aliyefuzu majaribio ambaye alisaini miaka miwili jana akitanguliwa na Feisal aliyesaini miaka mitatu.

Akizungumza mara baada ya kusaini Feisal alisema amefurahi kukamilisha uhamisho wake akitokea JKU na ni kama kukamilisha sehemu ya ndoto zake.

“Namshukuru Mungu kwa kufanikisha hatua hii, sasa naweza kusema mimi ni halali wa Yanga,” alisema.

Wakati huo huo, Yanga leo inacheza na Ashanti Uwanja wa Chuo cha Polisi.