Lipuli, Simba hapatoshi Iringa

Muktasari:

Hofu ya kuwapoteza nyota muhimu wa kikosi chake cha kwanza katika mechi hiyo dhidi ya Yanga kutokana na majeruhi ama adhabu ya kadi, huenda ikaiacha Simba kwenye wakati mgumu katika kuchagua wachezaji gani watakaocheza ama kutocheza kwenye mechi hiyo ya dhidi ya Lipuli.

Dar es Salaam. Mechi dhidi ya Yanga, Aprili 29 huenda ikaliweka mtegoni benchi la ufundi la Simba katika upangaji wa kikosi chake cha kwanza kwenye mechi muhimu dhidi ya Lipuli FC leo jioni kwenye Uwanja wa Samora, mkoani Iringa.

Hofu ya kuwapoteza nyota muhimu wa kikosi chake cha kwanza katika mechi hiyo dhidi ya Yanga kutokana na majeruhi ama adhabu ya kadi, huenda ikaiacha Simba kwenye wakati mgumu katika kuchagua wachezaji gani watakaocheza ama kutocheza kwenye mechi hiyo ya dhidi ya Lipuli.

Ni wazi kwamba pamoja na umuhimu wa pointi tatu za mchezo wa Lipuli, mechi ya Yanga ina uzito mkubwa kwa Simba kwani ndio inaweza kutoa taswira ya Ubingwa msimu huu lakini pia ni mchezo ambao mara kwa mara hugusa hisia za mashabiki na wapenzi wa soka nchi nzima.

Simba itamkosa Jonas Mkude ambaye anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano, lakini ipo kwenye mtihani wa kuamua iwatumie au kutowatumia nyota wake wawili tegemeo, kipa Aishi Manula na mshambuliaji Emmanuel Okwi.

Iwapo ikiwatumia wachezaji hao, kuna uwezekano mmoja au wote wawili wakaonyeshwa kadi za njano ambazo zitawafanya wakose mechi dhidi ya Yanga lakini uamuzi wa kuwaweka nje unaweza kupunguza nguvu ya timu kutokana na ufanisi wa wachezaji hao kwenye kikosi cha kwanza.

"Kikosi chote kilichosafiri kuja hapa Iringa kipo fiti na leo (jana) jioni tutafanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja ambao tutautumia kwa mechi hiyo kama kanuni zinavyofafanua ambayo yatakuwa ni mazoezi ya kucheza uwanja mzima. Mchezaji ambaye tutamkosa ni Mkude anayetumikia adhabu ya kadi tatu lakini wengine wote waliopo hapa wamo kwenye mipango yangu.

Kuhusu Okwi na Manula nafahamu kwamba hadi sasa wana kadi mbili za njano hivyo kama watapata kadi kwenye mechi hii watakosa mchezo dhidi ya Yanga lakini binafsi siko tayari kuweka nje wachezaji wangu wawili tegemeo kwa hofu ya kadi.

“Nitawapanga Okwi na Manula katika mchezo wa kesho (leo) na naamini wao ni wachezaji wanaojitambua hivyo hawatojihusisha na aina yoyote ya utovu wa nidhamu unaoweza kuwafanya wapate kadi ingawa nimepanga wasimalize dakika tisini kwa sababu nitawafanyia mabadiliko," alisema kocha wa Simba, Pierre Lechantre.

Ushindi dhidi ya Lipuli utaifanya Simba ifikishe pointi 61 ambazo zitakuwa 14 mbele ya Yanga inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 47 na Jumapili itakuwa kibaruani huko Mbeya kukabiliana na Mbeya City.

Hata hivyo, Simba hawapaswi kuidharau Lipuli iliyo nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi na pointi zake 31 kwani timu hiyo imekuwa ikionyesha kiwango bora pindi inapokutana na timu kubwa.

Katika mzunguko wa kwanza, Lipuli inayonolewa na wachezaji wa zamani wa Simba, Amri Said na Selemani Matola, ilizivimbia Simba na Yanga ugenini Dar es Salaam baada ya kutoka nazo sare ya bao 1-1 kwenye kila mechi baina yao.

Kibarua kwa Lipuli kitakuwa ni kudhibiti safu kali ya ushambuliaji ya Simba inayoundwa na John Bocco na Emmanuel Okwi ambayo wawili hao hadi sasa kwa pamoja wamefumania nyavu mara 33.

Makali hayo ya Okwi na Bocco ndio yamechangia kwa kiasi kikubwa kuifanya Simba isipoteze mchezo wowote kwenye Ligi Kuu hadi sasa, rekodi ambayo kocha wa Lipuli, Amri Said ametamba kuwa wataivunja.

"Tunawaheshimu Simba kama timu inayoongoza ligi na inafanya vizuri kwa sasa lakini mkakati wetu uko palepale ambao ni kuibuka na ushindi ili kuwatibulia rekodi yao ya kutofungwa kwenye ligi.

Tumefanya maandalizi mazuri ukizingatia kwamba tumetoka kupata ushindi kwenye mchezo wetu uliopita dhidi ya Singida United hivyo vijana wana hamasa na molali ya kufanya vizuri zaidi na kuweka heshima mbele ya Simba," alisema Said.

Mkoani Mbeya, kesho Jumapili, Mbeya City wataikaribisha Yanga ambayo imetoka kufuzu hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mechi ya mwisho waliyokutana na Mbeya City uwanjani hapo ambapo walifungwa mabao 2-1.

Ushindi pekee ndio unaoweza kuweka hai matumaini ya Yanga kutetea ubingwa msimu huu kwani iwapo wakipoteza kwa kufungwa au kutoka sare, huenda pengo la pointi baina yake na Simba likazidi kuongezeka na hivyo kujiweka katika mazingira finyu ya kuwa mabingwa wa Ligi Kuu msimu huu.