Yanga yaishtukia Simba mapema

Thursday October 12 2017

 

By HATIMU NAHEKA

MASHABIKI wa Yanga hawana amani kwa sasa mtaani, hii ni kutokana na chama lao kuanza Ligi Kuu kwa kusuasua, kiasi cha kuwapa nafasi wapinzani wao, Simba kuwacheka, lakini mabosi wa timu wameshtuka na kuanza kupiga hesabu mpya.

Mabosi hao wa Yanga wameshtukia mchezo mapema na kuweka hesabu zao sawa kabla ya kuvaana na Simba wiki mbili zijazo katika mchezo unaotajwa kuwa na hatma ya makocha wa pande zote mbili.

Yanga inacheza mechi mbili mfululizo zijazo ugenini wakianza na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba kisha watasafiri hadi Shinyanga kuivaa Stand United.

Ratiba hiyo, imewaamsha mabosi hao wa Yanga na kulazimika kupiga hesabu upya na kuamua kusafirisha kikosi chao angani badala ya kutumia barabara, hii ikiwa kuwafanya warejee Dar kuvaana na Simba wakiwa kamili gado Oktoba 28.

Mabingwa hao mara tatu mfululizo wa Ligi Kuu wameamua kusafiri kwa ndege kwenda Kanda ya Ziwa, huku ikiondoka na nyota wote isipokuwa Mzimbabwe Donald Ngoma pekee ambaye hata hivyo ataungana na wenzake baadaye.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa Yanga George Lwandamina amesema amelazimika kusafiri na kikosi kizima lengo likiwa ni kuwa na vijana wake wote kwa kuwa baada ya mechi hizo mbili watakutana na Simba.

Lwandamina alisema amefurahishwa na akili iliyopigwa na mabosi wa timu hiyo kwa kuamua kuisafirisha timu yao kwa ndege, uamuzi ambao utawapunguzia uchovu wachezaji wake ambao wangeweza kukutana na Simba wakiwa pia na uchovu.

“Nilikuwa napiga hesabu za safari ya kutoka hapa Dar es Salaam mpaka Bukoba, ni ndefu kwa basi, lakini nashukuru uamuzi wa uongozi kwa kubadili muundo wa safari hiyo,” alisema.

Simba na Yanga zitavaana kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam likiwa ni pambano lao la 99 katika Ligi Kuu tangu mwaka 1965, huku Yanga ikiwa na kumbukumbu ya kipigo cha mabao 2-1 katika mechi ya mwisho katika ligi hiyo.

Simba inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 11.