Yanga yaiburuza Simba ugenini

Dar es Salaam. Yanga imeiweka Simba kwenye wakati mgumu baada ya kukusanya pointi nne katika mechi mbili za ugenini wakati watani zao hao wakiwa wamepata mbili tu.

Yanga imecheza mechi mbili za ugenini msimu huu dhidi ya Njombe Mji na Majimaji wakati Simba imecheza dhidi ya Azam na Mbao FC.

Yanga ilipata pointi tatu dhidi ya Njombe Mji baada ya ushindi wa bao 1-0 kisha kupata pointi nyingine moja baada ya sare ya 1-1 na Majimaji.

Simba kwa upande wao walilazimishwa suluhu na Azam kisha sare ya mabao 2-2 na Mbao FC na kupata alama mbili tu ugenini.

Prisons ya Mbeya ndiyo inaongoza kwa kupata pointi nyingi ugenini baada ya kuzifunga Njombe Mji na Mwadui hivyo kupata alama sita.

Ndanda iko sawa na Yanga baada ya kupata alama nne kwa kuifunga Mbeya City na kisha kupata sare dhidi ya Prisons.

Timu nyingine zilizopata alama tatu ugenini msimu huu ni Mbao FC iliyoifunga Kagera Sugar 1-0, Azam FC iliyoifunga Ndanda 1-0 na Singida United iliyoshinda 1-0 dhidi ya Stand United.