Yanga yaambulia pesa ya chipsi kuku Shinyanga

Muktasari:

Si mnajua ni msosi wa harakaharaka na unaopendwa sana na masela pamoja na sista du. Kwanza bei yake ni rahisi, pia upatikanaji wake ni wa fasta mtaani, sasa we fikiria kwa klabu kubwa kama Yanga inawezaje kuambulia mapato ya nunulia msosi huo?

HUWEZI kuamini lakini ndivyo ukweli ulivyo. Yanga inapigwa uwanjani, huku kipa wao Youthe Rostand akizidi kuchekesha kwa mabao anayofungwa, lakini klabu hiyo inatia huruma zaidi baada ya kujikuta ikiambulia pesa kiasi cha kununulia chips kuku tu.

Si mnajua ni msosi wa harakaharaka na unaopendwa sana na masela pamoja na sista du. Kwanza bei yake ni rahisi, pia upatikanaji wake ni wa fasta mtaani, sasa we fikiria kwa klabu kubwa kama Yanga inawezaje kuambulia mapato ya nunulia msosi huo?

Ni hivi. Yanga imejikuta ikitia huruma mikoani kwa kuambulia mapato kiduchu kwani unaambiwa mechi yao ya juzi waliolala 1-0 mbele ya Mwadui FC baada ya kuvuna Sh100,000 tu. Ndio Laki Moja tu, huku mchezo wao na Mtibwa Sugar waliolala pia 1-0 mjini Morogoro walivuna mapato ya Sh300,000.

Kwa mujibu wa chanzo cha ndani ya Yanga kinasema hali ya mapato kwa sasa katika klabu hiyo imezidi kushuka baada ya kuambulia kiasi cha Sh468,000 ndani ya mechi hizo ikiwa ni rekodi mpya kwao.

Anguko hilo baya kwa Yanga kimapato lilianza kuonekana katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar na Yanga iliambulia kiasi cha Sh358,000, kabla ya juzi mjini Shinyanga kuvuna mapato ya Sh110,000 ambao mshua anaweza kununua chips kuku na kuimaliza.

Chanzo kikubwa cha mapato hayo kilionekana kuwa ni mashabiki kukata tamaa na ubora wa timu yao hasa baada ya kupoteza mchezo uliotangulia dhidi ya Prisons huku kikosi hicho kikiwa kimegawanywa mara mbili.

Hata hivyo, Yanga inaambulia pato hilo kiduchu kutokana na klabu hiyo kukatwa madeni mbalimbali ya kodi ya ardhi na kuwalipa Katibu Mkuu wake wa zamani Celestine Mwesigwa na aliyekuwa msemaji wao, Louis Sendeu kutokana na amri ya mahakama.