Yanga wataumia sana

Muktasari:

  • Kipigo hicho cha mabao 4-0 ilichokipata ugenini jijini Nairobi, Kenya mbele ya wababe wa huko, Gor Mahia, kimezidi kufifisha nafasi ya Wana Jangwani hao kusonga mbele kutokea Kundi D lenye pia timu za USM Alger ya Algeria na Rayon Sports ya Rwanda ambayo nayo ilikubali kichapo cha mabao 2-1 nyumbani kwao hiyo juzi pia.

KIZA kinene. Kiza kizito. Ndicho unavyoweza kuielekezea Yanga katika safari yake kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kipigo ilichokumbana nacho juzi Jumatano usiku.

Kipigo hicho cha mabao 4-0 ilichokipata ugenini jijini Nairobi, Kenya mbele ya wababe wa huko, Gor Mahia, kimezidi kufifisha nafasi ya Wana Jangwani hao kusonga mbele kutokea Kundi D lenye pia timu za USM Alger ya Algeria na Rayon Sports ya Rwanda ambayo nayo ilikubali kichapo cha mabao 2-1 nyumbani kwao hiyo juzi pia.

Mwanaspoti kama ilivyo kawaida, lilikuwepo jijini Nairobi kufuatilia kwa ukaribu kabisa mechi ya Yanga na Gor iliyofanyika uwanjani Kasarani na hapa linakuletea tathimini ya kila mchezaji wa Yanga alivyocheza.

Youthe Rostand

Unaweza kushangaa hili, lakini ndio ukweli wenyewe. Ni kwamba kipa huyu juzi alikuwa kwenye ubora wake pamoja na kwamba nyavu zake zilitikiswa mara nne. Kama asingekuwa katika ubora huo, Yanga ingeweza kufungwa mengi zaidi.

Achana na hayo mabao manne, lakini Rostand aliokoa mipira mingi iliyokuwa inatinga nyavuni. Washambuliaji wa Gor wakiongozwa na Jacques Tuyisenge (kabla ya kuumia na kutoka) waliliandama mno lango hilo. Mara nyingi Rostand hufungwa mabao ya kizembe, lakini mbele ya Gor kwanza alijirekebisha udhaifu wake wa kutocheza mipira ya krosi huku akiongeza umakini kwa asilimia kubwa.

Juma Abdul

Alicheza beki ya kulia baada ya kukosekana Hassan Kessy ambaye bado hajawekana sawa na uongozi wa klabu hiyo katika suala la mkataba mpya.

Abdul ambaye ndiye alikuwa nahodha, katika mechi hii hakucheza kwa kiwango cha juu, pengine kwa kutotumika kwake kwa muda mrefu kwenye mechi za kimashindano.

Francis Kahata, winga wa Gor alikuwa mwiba katika mechi akimgeuza Abdul uchochoro, japo shughuli aliipata.

Lakini ni ukweli usiopinga Abdul hakuwa fiti. Hakuwa katika ule ubora wake wa kupiga krosi kali na tamu ambazo huhitaji mtu wa kujirusha tu mpira ujae kambani. Mpaka filimbi ya mwisho hakufanya hivyo.

Gadiel Michael

Alikuwa beki wa kushoto, naye hakuwa bora katika kiwango, pengine kutokana na kwamba walishambuliwa muda mwingi.

Gadiel ambaye amezoeleka katika kutengeneza mashambulizi kupitia upande wake huo, lakini alimudu kuchonga krosi za maana mbili tu kipindi cha kwanza. Mara nyingine alipokonywa mipira huku pia akikumbana na faulo za kutosha tu.

Kati ya wachezaji wa Yanga ambao walishindwa kutamba katika mechi hii, Gadiel, yumo. Ijapokuwa alizimaliza dakika zote 90 tisini, lakini ni wazi mchezo ulimzidi uwezo.

Abdallah Shaibu ‘Ninja’

Kwanza hana uzoefu wa kucheza mechi nyingi za kimashindano katika kikosi cha Yanga, lakini angalau yeye alionyesha kiwango kidogo, achilia mbali makosa ya hapa na pale ya kimchezo aliyoyafanya.

Ninja hakucheza kwa maelewano na beki mwenzake wa kati na kujikuta wakifanya makosa mengi ambayo yaliwaghalimu kufungwa mabao hayo manne.

Mapungufu yalikuwa mengi katika nafasi ya beki wa kati lakini Ninja aliweza kuwamudu mastraika wa Gor mara kadhaa. Jinsi alivyocheza Inashawishi kuamini kwamba alichangia kupunguza kipigo, ni kama alivyofanya Rostand.

Adrew Vicent ‘Dante’

Pengine kutokufanya mazoezi ya pamoja na timu wakati ikijiandaa kwa ajili ya mchezo huu kulimuondoa katika ubora wake. Hili lilionekana wazi baada ya mara kadhaa kuzidiwa ujanja na Tuyisenge.

Dante wa juzi mbele ya Gor hakuwa yule mwenye uwezo wa kupiga au kuokoa kwa kutumia kichwa, mguu wowote akicheza kwa akili. Kabla ya mechi kuanza, matumaini makubwa ya Yanga haswa katika nafasi ya ulinzi yalikuwa kwa Dante. Ilitegemewa kwa uzoefu wake angeituliza timu isifanye makosa mengi. Lakini hali ikawa tofauti. Dante alihusika katika makosa mengi.

Haji Mwinyi

Kwa Yanga imezoeleka kwamba katika nafasi ya kiungo mkabaji kama usipomwona Kabamba Tshishimbi, basi atakuwepo Saidi Juma Makapu, lakini juzi ikawa tofauti.

Kocha Mkongomani Mwinyi Zahera, aliamua kumwanzisha Mwinyi ambaye kiasili hiyo si nafasi yake. Yeye hucheza beki ya kulia.

Mwinyi hakuwa na sifa za kiungo mkabaji, alizidiwa na viungo wa Gor Mahia waliotamba katika eneo hilo katika dakika zote ambazo Mwinyi alicheza kabla ya kutolewa.

Makosa ya kutokukaba katikati ya uwanja ambapo Mwinyi alicheza, yalisababisha kupigwa pasi mbili za maana kipindi cha kwanza na zote zilitumiwa vyema na Gor kufunga mabao mawili.

Hakuwa na sifa ya kucheza katika nafasi hii, lakini hata kiwango chake hakikuwa bora.

Ibrahim Ajibu

Alikuwa winga wa kulia kwa dakika 77 alizocheza. Hakuwa na msaada kwa timu kwenye kukaba, kibaya zaidi hata alipopa mipira, mara nyingi aliipoteza kwa kupiga pasi zilizonaswa na wapinzani kirahisi.

Ajibu anajulikana kwa ubora wake wa kuchezea mpira, kutengeneza nafasi za kufunga au hata kufunga mwenyewe, lakini hayo yote juzi hayakuonekana kwake. Tena mbaya zaidi, mabeki wa Gor Mahia wala hawakupata shida kumtuliza.

Mara nyigine alicheza kibinafsi kwa kulazimisha kupiga chenga hata katika mazingira ambayo hakuwa na ulazima wa kufanya hivyo.

Kabamba Tshishimbi

Alikuwa na shughuli nzito akilazimika kuibeba timu mabegani. Viungo wa Gor ni kama walimjua mapema, walijipanga dhidi yake na hakika walimbana ijapokuwa aliweza kupiga pasi fupi na ndefu mara nyingi tu japo zilishindwa kutumiwa vyema na wenzake.

Alikuwa katika kiwango chake lakini alikosa msaada kutoka kwa mawinga wa pande zote na kiungo mkabaji, Mwinyi.

Kocha wa Gor Mahia, Dylan Kerr, mara kadhaa aliwafokea wachezaji wake kwa namna walivyoshindwa kumbana Tshishimbi. Mkongomani huyo alijitahidi, wenzake walimwangusha.

Yohana Mkomola

Kwa kifupi unaweza kusema mechi ilikuwa kubwa kwake. Ilimpwaya ya kutosha. Inawezekana ni kutokana na kutoka kwake benchi la majeruhi alilokalia kwa muda mrefu kiasi cha kushindwa kucheza mechi nyingi za kimashindano za Yanga na timu ya taifa ya vijana ya U-20, Ngorongoro Heroes.

Kwa dakika 54 alizokuwa uwanjani, hakufanya shambulizi lolote la maana wala kupiga shuti lililolenga lango.

Yanga ililazika kuanza na Mkomola katika nafasi hiyo kwani hakukuwa na straika wa kuanza baada ya Amissi Tambwe kuwa majeruhi zaidi yake.

Badala ya kushambulia, alijikuta akiwekwa mfukoni na mabeki wa Gor na kushindwa kufanya lolote.

Juma Mahadhi

Si mchezaji wa kikosi cha kwanza kikosini humo, lakini kutokana na mapungufu ya wachezajia ambayo Yanga imekumbana nayo kipindi hiki, amekuwa akitumika nafasi ya straika.

Kila wakati Mahadhi alipopata mpira, mbele yake aliwakuta mabeki watatu au wawili na walimmudu. Hivyo hakuweza kufanya lolote la maana ingawa alicheza dakika zote.

Hakuwa Mahadhi yule wa enzi anasajiliwa Yanga akitokea Coastal Union. Kuna nyakati alipata nafasi ya kupiga mashuti, lakini hakuweza kulenga lango.

Pius Buswita

Hakuonekana kwenye ubora wa kuanzisha mashambulizi. Mbele ya Gor alicheza zaidi wingi ya kushoto na hakutamba kwa lolote. Buswita hakuwa bora katika kukaba wala kushambulia na hakuweza kupiga krosi yoyote iliyoenda shule.

WALIOINGIA NAO

Katika mechi hiyo, Yanga ilifanya mabadiliko matatu. Said Mussa aliingia kuchukua nafasi ya Mkomola dakika ya 54, naye alishindwa kubadili mchezo, zaidi Gor wakatumia upande alipokuwapo kupitishia mashambulizi wao. Mussa bado ni kijana, ni wazi asingeweza kuhimili presha ya mechi hiyo.

Emmanuel Martine yeye aliingia dakika ya 77 akimbadili Ajibu, naye yalikuwa yale yale. Mkongwe Tambwe aliingia dakika ya 80 kuchukua nafasi ya Mwinyi. Tambwe hajarejea kwenye makali bado, mzimu wa majeruhi bado haujamwacha salama.