Yanga wamteka Ngoma airport

Muktasari:

Lakini Simba na wenyewe wanakomaa kwa vile tajiri yao na wasaidizi wake inadaiwa wamezungumza na Ngoma na amewaambia kwamba leo ndio anasaini kumaliza ishu. Simba wanaamini kuwa wakimtia Ngoma mikononi kwa dakika chache tu wanampa chake na biashara imeisha.

KUNA kitu kinaendelea Dar es Salaam. Leo Jumanne kutakuwa na mchuano mkali baina ya vigogo wa Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam, kila mmoja akimwwania Donald Ngoma.

Yanga wamesikia kwamba mchezaji huyo ameshapata ushawishi mkubwa na ameridhia kusaini Msimbazi, ndio maana wameamua kukomaa na leo wamedai kuwa watakinukisha Uwanja wa Ndege waondoke naye kwani amewaambia anarudi Dar es Salaam kwa ajili yao na si Simba.

Lakini Simba na wenyewe wanakomaa kwa vile tajiri yao na wasaidizi wake inadaiwa wamezungumza na Ngoma na amewaambia kwamba leo ndio anasaini kumaliza ishu. Simba wanaamini kuwa wakimtia Ngoma mikononi kwa dakika chache tu wanampa chake na biashara imeisha.

Mchezaji huyo hajasaini popote zaidi ya kuzungumza kwenye simu na kuchat Whatsapp, lakini Simba wamepania kumnasa si tu kuwaziba midomo Yanga, lakini kuboresha safu yao ya ushambuliaji tayari kwa Kombe la Shirikisho mwakani huku Yanga wakifikiria hivyo hivyo kwenye Ligi ya Mabingwa.

Habari zinasema kwamba Ngoma alikubaliana na Simba mambo mengi, lakini wamepatwa na mshtuko kuwa Yanga inaweza kupindua meza dakika yoyote kwavile wao Simba hawajamtia mikononi. Yanga wanasisitiza kwamba si Ngoma wala Amissi Tambwe anayeondoka Jangwani.  Tambwe amerejea nchini akitokea kwao Burundi ambapo juzi alikuwa na kikao kizito na uongozi wa Yanga makao makuu ya klabu hiyo Jangwani.

Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa alisema: “Ngoma ni mchezaji wa Yanga hadi Julai atakapomaliza mkataba, lakini pia tumeshazungumza naye na tumekubaliana atabaki Yanga na yuko kwenye programu za kocha msimu ujao.

“Tunao wachezaji watatu wa kigeni ambao tutawaongezea mikataba kipindi hiki.”Hata hivyo  Mkwasa aligoma kuwataja majina kwa madai kwamba wamewaandalia utaratibu maalumu wa kuwatambulisha.

Hata hivyo, habari za ndani zinaeleza kwamba miongoni mwa wachezaji hao ni Tambwe na Ngoma ambao wako katika hatua za mwisho mwisho za kusaini mikataba mipya ingawa lolote linaweza kutokea kutokana na hali ya kiuchumi kudorora Yanga.

Kiongozi huyo alifafanua hatma ya mchezaji Vicent Bossou kwa kusema: “Bossou hatokuwepo, Yanga ilipenda kuendelea naye lakini tatizo ni mchezaji mwenyewe amekataa kuongeza mkataba.”

Mbali na Bossou, tayari Yanga imeachana na kiungo wake Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, ambaye kulikuwa na tetesi za kushindwana naye kwenye maslahi na Justin Zullu ‘Mkata Umeme’ ambaye hakuwa na msimu mzuri tangu alipotua.