Wanajeshi kuzijaribu silaha za Yanga kesho

Tabora. Mabingwa wa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga itacheza mechi yake ya kirafiki dhidi ya Rhino Rangers kesho, Jumatano kwenye Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi Mkoani Tabora.
Yanga imeweka kambi mkoani hapo kujiandaa na  mchezo wake wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand United utakaochezwa mwishoni mwa wiki kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Akizungumzia mchezo dhidi ya Rhino, Kaimu afisa habari wa Yanga, Godlisten Anderson 'Chicharito' amesema mchezo huo utakuwa ni fursa ya mashabiki wa Tabora kuiona timu yao msimu huu.
Chicharito alisema mbali na kutoa fursa hiyo ya mashabiki kuwaona wachezaji wao pia wataitumia mechi hiyo ikiwa ni sehemu ya benchi la ufundi kuangalia utayari wa kikosi chao kabla ya kwenda kuifuata Stand United watakaokutana nao Jumapili Oktoba 22, Mkoani Shinyanga.
"Timu yetu imeweka kambi hapa ikitaka kujiandaa kwa utulivu kabla ya kukutana na Stand United lakini hii ni nafasi kwa benchi la ufundi kuwapima hata wale ambao hawakupata nafasi ya kucheza mchezo wa mwisho dhidi ya Kagera Sugar wiki iliyopita," alisema Chicharito.
Kocha msaidizi wa Rhino, Hamady Mgongo alisema wanatarajia kupata kipimo kizuri kutoka kwa Yanga kabla ya mchezo wao dhidi ya Toto African ya Mwanza katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza.
"Tunatarajia mechi nzuri ya kesho kama unavyojua wenzetu wapo katika ligi kama ilivyo sisi hatutawahofia tunaingia kwa kupambana nao ili tuweze kuwafunga, tukifanikiwa hilo imani yetu kwamba litaongeza morali kwa vijana wetu kabla ya mchezo wetu dhidi ya Toto," alisema Mgongo.