Yanga ikitumia mbinu hizi URA hatoki

‘Nguvu yetu ni kuangalia ni jinsi gani ambavyo tunaweza kuwazidi wapinzani wetu URA, nimewaona wana timu ya ushindani na hata kufika hapo walistahili’

Shedrack Nsajigwa.

Zanzibar. Yanga leo inatakiwa kucheza mpira wa pasi za chini, kushambulia kwa nguvu na kutowapa nafasi URA ya Uganda kusogea katika lango lao, kama inataka kupata ushindi katika mchezo huo.

Yanga inatakiwa kutumia mbinu hiyo kwa kuwa wapinzani wao ni warefu na wanatumia mipira ya juu kupeleka mashambulizi ya kasi langoni mwa wapinzani wao.

Timu hizo zinavaana katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi unaotarajiwa kuanza saa 10:30 jioni kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Baadaye timu za Tanzania Bara,  Azam na Singada United zitapepetana katika mchezo wa nusu fainali ya pili itakayochezwa saa 2:30 usiku.

Yanga inatakiwa kuwa makini kwa kuwa URA ni timu inatumia mfumo wa kushambulia na kulinda lango kwa pamoja jambo ambalo mabingwa hao wa Ligi Kuu wanatakiwa kujipanga kikamilifu.

URA ina wachezaji wenye maumbo makubwa kuliko Yanga, hivyo ikitaka kushambulia kwa mipira ya juu kama ilivyocheza katika mechi zake zilizopita itapata taabu kupata ushindi.

URA ilikuwa kinara wa Kundi A kwa pointi 10, Azam (9), Simba (4), Mwenge (4) na Jamhuri pointi moja. Singida United iliongoza Kundi B baada ya kuvuna pointi 13 sawa na Yanga lakini ina uwiano mzuri wa idadi ya mabao, Mwenge (6), JKU (4), Taifa ya Jang’ombe (4) na Zimamoto (3).

Yanga imefika nusu fainali ikiwa imara katika eneo la kiungo ikinogeshwa na Papy Tshishimbi,  Pius Buswita,  Raphael Daud, Pato Ngonyani, Said Juma ‘Makapu’ na Maka Edward.

Yanga ipo vizuri licha ya kuwakosa nyota kadhaa, lakini wachezaji ambao hawapati namba kikosi cha kwanza wamekuwa kwenye kiwango bora na mabao sita waliyofunga yametokana na kazi nzuri.

Juma Mahadhi alifunga mawili, Ibrahim Ajibu, Yohana Nkomola, Hassani Kessy na Makapu walifunga bao moja kila mmoja. Yanga haikuwa na kina Obrey Chirwa, Donald Ngoma,  Amiss Tambwe na Thabani Kamusoko.

Katika nusu fainali ya Singida United dhidi ya Azam, utakuwa mchezo ngumu kutokana kwa kuwa wachezaji wengi wanafahamiana wakicheza katika ligi.

Kocha  msaidizi wa Yanga Shedrack Nsajigwa alisema wanashukuru wachezaji wake wamejituma na kuingia katika hatua ya nusu fainali ambayo watapambana kupata ushindi.

“Nguvu yetu ni kuangalia jinsi gani ambavyo tunaweza kuwazidi wapinzani wetu URA, nimewaona wana timu nzuri ya ushindani na hata kufika hapo walistahili, “ alisema Nsajigwa.

Kocha wa URA, Nkata Paul alisema Yanga ni timu nzuri lakini wao ni bora zaidi na wamefika fainali baada ya kucheza  vyema katika mechi za awali.