Yanga ikifungwa, Madee anavurugwa

MSANII wa kizazi kipya, Hamad Ally ‘Madee’

MSANII wa kizazi kipya, Hamad Ally ‘Madee’ kumbe ni Yanga lialia bwana na pale wana Jangwani hao wanapochapwa uwanjani hukosa raha kabisa. Lakini kuelekea mechi ya Ngao ya Jamii ya Jumatano ijayo ambapo timu yake itaumana na Simba, amesema nyota ya Ibrahim Ajibu itang’aa.

Madee amesema Ajibu ana nafasi kubwa ya kufanya vema katika mchezo huo ili kuwaonyesha mashabiki kuwa ana amani tosha ndani ya kikosi cha Yanga tofauti na wao wanavyodhani.

“Siku ile anatambulishwa Yanga watu walizusha eti hakuweza kuzungumza kwa kuwa alifanya maamuzi ya kukurupuka kuondoka Simba. Naamini kupitia mchezo huu atawajibu kwa vitendo, hivyo nyota yake itang’aa,” alisema.

Msanii huyo alisema anashangilia Yanga, timu ya kijanja yenye maendeleo ya kutwaa mataji ya ubingwa wa ligi.

“Naamini katika Ngao ya Jamii Yanga itafanya vema japokuwa itawalazimu kujituma, unajua Simba nao wanajipanga kutokana na jinsi walivyosajili, lakini Yanga ni Yanga itashinda tu,” alisema.