Yanga ebwana ndio!

Muktasari:

Mwimbaji huyo anajaribu kutaja sifa za mwanamume, lakini buana katika Ligi Kuu Bara kwa mechi za raundi ya sita, Yanga wamethibitisha kuwa wao ni mashine.

MKALI wa miondoko ya Singeli, Msaga Sumu anakimbiza nchini na songi lake tamu la Mwanaume Mashine’. Mwimbaji huyo anajaribu kutaja sifa za mwanamume, lakini buana katika Ligi Kuu Bara kwa mechi za raundi ya sita, Yanga wamethibitisha kuwa wao ni mashine.

Watetezi hao sio timu ya mchezo mchezo. Imethibitisha hilo wikiendi iliyomalizika baada ya kuwa timu pekee kati ya 16 iliyopata ushindi, tena ugenini.

Iliifunga Kagera Sugar 2-1 Uwanja wa Kaitaba, Bukoba na kuweka rekodi hiyo ya maana kwa mabao ya Ibrahim Ajibu na Obrey Chirwa akifunga bao lake la akwanza msimu huu, huku la Kagera likifungwa na Jafar Kibaya.

Kwa matokeo hayo Yanga sasa ina alama 12 sawa na vinara Simba pamoja na Azam na Mtibwa Sugar lakini tofauti ipo katika mabao ya kufunga na kufungwa.

Zikiwa zimechezwa mechi sita sasa, mambo kadhaa yanazidi kujifunua na kutoa taswira ya namna msimu utakavyokuwa.

Ligi ni ngumu

Matokeo ya mechi za wikiendi yametosha kuonyesha msimu huu utakavyokuwa mgumu. Kwanza hakuna timu iliyokuwa nyumbani ambayo imepata ushindi. Mbao walilazimishwa sare na Mbeya City. Mwadui wakalazimishwa sare na Azam, Ruvu Shooting wakasuluhu na Singida United, Prisons ikasuluhu na Stand United sawa na Njombe Mji na Lipuli. Kagera iliyokuwa nyumbani ilipoteza kwa Yanga, wakati Ndanda ililazimishwa sare na Majimaji. Inashtua kidogo.

Katika hali ya kawaida timu inayocheza nyumbani inakuwa na nafasi kubwa ya kushinda, lakini wikiendi hii haikuwa hivyo. Timu zilizokuwa nyumbani zilipata wakati mgumu. Hata Simba yenye kikosi cha Sh1.3 bilioni ilijikomboa dakika za mwisho kutoka katika midomo ya Mtibwa Sugar.

Ajibu kawa mtamu

Kuna Ibrahim Ajibu mmoja tu Ligi Kuu. Ni yule aliyecheza dhidi ya Kagera Sugar. Ajibu amezidi kunoga ndani ya Yanga. Anaufanyia mpira anachotaka, tena katika hali ya kujiamini mno. Kuna mchezaji gani anafanya kama yeye? Hakuna.

Kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar alitoa pasi ya bao kwa Obrey Chirwa, tena pasi ya maana. Kipindi cha pili akatulia na kufunga bao murua la ushindi.

Ajibu amenoga kweli kweli. Mbali na kupiga mashuti na kutengeneza nafasi, pia ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kuwa hatari kwa wapinzani. Hakuna beki anayejiachia pindi akicheza na Ajibu. Mechi sita mabao matatu, anakwenda vizuri.

Mbeya City ni moto

Mbeya City imerudi, tena kivingine kabisa. Wikiendi iliyomalizika ilitosha kuthibitisha hilo. Katika kipindi cha kwanza tu, ilishakubali kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Mbao. Kila mdau wa soka aliamini mechi imekwisha.

Nani kasema Mbeya inapoteza mchezo kirahisi hivyo? Mbeya City walituliza kichwa. Wakaishambulia Mbao kama wanafunzi wanaovamia shamba la miwa. Mbao ikalegea na kukubali mabao yote mawili kurudi. Huwa inatokea mara chache sana.

Hii haikuwa mara ya kwanza kwa City kutoka nyuma na kupata matokeo. Mechi iliyopita dhidi ya Mwadui walitoka pia nyuma na kupata sare. Straika wao mtata, Eliud Ambokile amezidi kudhihirisha hatanii na anafanya kweli. Alifunga bao lake la tatu msimu huu dhidi ya Mbao. Yuko vizuri.

Tuitazame Mtibwa vizuri

Mtibwa hii inaonekana kuwa vizuri zaidi. Juzi Jumapili walicheza mechi ya 14 mfululizo bila kupoteza. Mechi ya mwisho walifungwa Februari 5 na Mbao FC. Sio Simba, Yanga wala Azam yenye rekodi kama hiyo.

Katika mechi hizo imecheza na Yanga mara mbili, Dar es Salaam na Morogoro, na Simba mara mbili, Dar es Salaam na Morogoro. Zote hizi hawajapoteza. Ni timu chache zenye uwezo huo.

Pia juzi Jumapili Mtibwa ilipata pointi moja dhidi ya Simba jijini Dar es Salaam kwa mara ya kwanza tangu 2012. Ipo vizuri.

Kabange anamuumbua mtu

Kocha wa Njombe Mji, Mrage Kabange anazidi kumuumbua bosi wake wa zamani, Hassan Banyai, baada ya kuiongoza timu hiyo ya Nyanda za Juu Kusini katika mechi tatu bila kupoteza. Ni rekodi ya maana. Banyai ambaye alibwaga manyanga wiki chache nyuma, alidai hata aende kocha gani Njombe, timu hiyo haitaweza kupata matokeo mazuri.

Hata hivyo, mambo yamekuwa tofauti. Kabange ameonyesha inawezekana. Njombe sasa haifungiki kirahisi tena. Wikiendi iliyomalizika ilisuluhu na Lipuli na kufikisha alama tano.

Maxime kunani?

Mecky Mexime anataabika jamani. Mechi ya sita msimu huu bila ushindi wowote. Inasikitisha sana kuona hali kama hiyo inamtokea aliyekuwa kocha bora zaidi msimu uliopita. Kipigo kutoka kwa Yanga kimezidi kumchimbia Mexime kaburi. Hakuna namna sasa Mexime inabidi apambane na hali yake. Matokeo yoyote mabaya katika michezo inayofuata yanaweza kuhitimisha ajira yake ndani ya Kagera Sugar. Hatma ya Kagera sasa ipo mikononi mwake.

Shaaban Nditi huyu

Kuna watu wana historia za kipekee. Nahodha wa Mtibwa Sugar, Shaaban Nditi, juzi Jumapili aliivuruga safu ya kiungo ya Simba, akicheza sambamba na viungo wengine Saleh Abdallah na Mohammed Issa. Unajua Nditi ana historia gani?

Alisajiliwa na Simba 2004 lakini baada ya muda mfupi wakamtema na kwa madai ni mzee. Miaka 13 baadaye bado yupo katika ubora wake. Simba imesajili viungo zaidi ya 15 lakini bado Nditi yupo vile vile. Soka wakati mwingine lina vituko sana.