Yanga bingwa mteule

Muktasari:

Bao la dakika ya 81 lililofungwa na Amissi Tambwe kwa kichwa akiunganisha krosi safi ya Juma Abdul lilitosha kuipa Yanga ushindi na kuwahakikishia ubingwa huku Mrundi huyo akifikisha bao la 11 msimu huu.

Dar es Salaam. Yanga imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya kuifunga Toto African bao 1-0 katika mchezo mkali uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Bao la dakika ya 81 lililofungwa na Amissi Tambwe kwa kichwa akiunganisha krosi safi ya Juma Abdul lilitosha kuipa Yanga ushindi na kuwahakikishia ubingwa huku Mrundi huyo akifikisha bao la 11 msimu huu.
 Kutokana na matokeo hayo Yanga imefikisha pointi 68 huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi dhidi ya Mbao Jumapili, lakini mabao mengi ya kufunga yanaibeba timu hiyo hata kama Simba itaifunga Mwadui Jumapili.

Simba yenye pointi 65 ikiifunga Mwadui itafikisha pointi 68 lakini idadi ndogo ya mabao iliyofunga msimu huu (mabao 48) yameipa nafasi Yanga kutwaa ubingwa ikiwa na mchezo mkononi kutokana na kufunga mabao 59, mabao ambayo Simba hawawezi kuyafikia.
Timu zote zilianza mchezo kwa kasi, lakini Toto walionekana kuidhibiti vilivyo Yanga dakika 45 za kipindi cha kwanza na kwenda mapumziko timu hizo zikiwa 0-0.
Kipindi cha pili Yanga walirejea kivingine na kufanya mashabulizi ya kushutukiza kupitia kwa mabeki wa pembeni, lakini uimara wa kipa wa Toto,  David Kissu ulikuwa kikwazo kwa washambuliaji wa Yanga.
Kipa  wa Toto African, Kissu alijikuta akiangua kilio baada ya filimbi ya mwamuzi na  kusaidiwa kunyanyuka na viongozi wa timu yake walioenda kumpoza machungu.
Sasa Toto African italazimika kushinda mchezo wake wa mwisho dhidi ya Mtibwa Sugar, pia iombee Yanga iifunge Mbao na Ndanda ipoteze dhidi ya JKT Ruvu ili yenyewe ibaki kwenye ligi msimu ujao.