Yanga Bongo inapiga tu!

Muktasari:

  • Baada ya shambulio hilo Yanga wamekuwa wakienda golini kwa African Lyon lakini walishindwa kutengeneza nafasi ya kufunga.

Dar es Salaam. Kikosi cha Yanga kimetoka kifua mbele baada ya kuwafunga African Lyon bao 1-0, katika mchezo wa kirafiki uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika dakika 45 za mwanzo, Yanga walionekana kutawala mpira kwa kupiga pasi nyingi lakini tatizo lilikuwa kwenye kufunga tu.

Dakika ya 27, Mrisho Ngassa alipokea krosi safi ambayo alitokana na mpira wa faulo ambao ulipigwa na beki wa kushoto Gustapha Saimon ambayo aliunganisha kwa kichwa na kugonga mwamba.

Baada ya shambulio hilo Yanga wamekuwa wakienda golini kwa African Lyon lakini walishindwa kutengeneza nafasi ya kufunga.

Straika matata ya Yanga ambaye ametoka majeruhi, Mkongo Herieter Makambo alionekana kudhibitiwa vizuri na mabeki wa Lyon ambao waliweza kumaliza kipindi cha kwanza bila kuruhusu bao.

Makambo alipanwa na akawa anapokea mpira mbele ya mabeki wawili na hata alipopata nafasi ya kupiga shuti walinzi wa Lyon walizuia.

Yanga walipiga mashuti sita kupitia kwa Raphael Daud, Pius Buswita, Feisal Salum na Makambo ambayo yote hayakulenga lango na kutoka nje.

African Lyon wao walikuwa wakifanya mashambulizi ya kushtukiza tofauti na Yanga wakimtumia mshambuliaji aliyetamba na Simba, Haruna Moshi 'Boban' aliyekuwa akitengeneza nafasi ambazo nazo hazikuwa na madhara.

Licha ya Yanga kutawala mpira kwa muda mrefu, Lyon walikuwa makini zaidi katika kushambulia na nidhamu kubwa ya kukaba.

Umakini mkubwa wa kukaba ndani ya dakika 45, za kipindi cha kwanza African Lyon waliweza kuwazuia washambuliaji wa Yanga kuonekana wa kawaida tu.

Makambo, Ngassa, Daud, Buswita na Deus Kaseke walishindwa kupenya ngoma hiyo. 

 

KIPINDI CHA PILI

Yanga walifanya mabadiliko alitoka Raphael Daud na kuingia Papy Kabamba 'Tshishimbi' na Buswita nafasi yake ilichukuliwa na Matheo Anthony, pia dakika 63, alitoka Ngassa na kuingia, Mhilu.

Mhilu alihangaika huku na kule akiisaidia timu yake katika kukaba mpira inapopotea  na kushambulia wanapopata nafasi tofauti na ilivyokuwa kwa Ngassa ambaye alikuwa  akionekana wakati Yanga wanapomiliki mpira.

Dakika ya 76, Yanga walifanya mabadiliko kwa mara nyingine wakimtoa, Saimon, Kaseke na Makambo ambao nafasi zao zilichukuliwa na Jafary Mohammed, Ibrahim Ajibu na Mrundi Amiss Tambwe.

Mabadiliko hayo yalizaa matunda kwani Yanga walibadilika, walitengeneza nafasi sambamba na kushambulia mara kwa mara na kufanikiwa kupachika bao hilo katika dakika ya 83, kupitia kwa Mhilu ikiwa ni dakika 20, tu tangu aingie kuchukua nafasi ya Ngassa.

Mhilu aliunganisha mpira wa kichwa uliotemwa na kipa wa African Lyon alipokuwa anajaribu kupangua krosi ya Ajibu hata hivyo, African Lyon mbali ya kufanya mabadiliko walishindwa kubadilisha matokeo.

Mshambuliaji wao, Haruna Moshi 'Boban' alionekana kuwa mwiba kwa Yanga akitengeneza nafasi kwa kupiga pasi za mwisho na kusababisha hatari.