Yanga: Tutanunua beki kwa pesa yoyote

Friday August 11 2017

 

By KHATIMU NAHEKA

SIMBA bado wanatamba kwamba mwaka huu wanakikosi cha kumfunga yoyote tena nyingi tu wakiringia usajili wao wa majina makubwa lakini Yanga kumbe imetulia na kuangalia hilo kisha wakatamka kwamba wanachoshukuru ni kukiona kikosi hicho cha watani wao na sasa wanamalizia kazi moja kisha watakuwa tayari kuubishia usajili huo.

Aliyeyazungumza hayo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga Hussein Nyika ambaye ameliambia Mwanaspoti kuwa wala hawana wasiwasi juu ya usajili huo wa Simba na kwamba kwao imekuwa nafuu kubwa kukiona kikosi hicho kilichowashusha presha.

Nyika amesema dakika yoyote watashusha nchini beki la haja kwa gharama yoyote ile na kwenye mechi ya watani wa jadi atacheza.

“Unajua mimi sioni kama kuna sababu ya Wanayanga kuumiza kichwa juu ya kelele za Simba kuna wakati hata mimi nilikuwa  naumiza kichwa juu ya usajili wao lakini tukagundua kwamba hatuna sababu ya kuhofia,”alisema Nyika. “Simba imerudi na tumeiona,unapokuwa unajua soka hauna sababu ya kuongea kauli za kishabiki,watu wanatakiwa kufahamu hatukuwa na kikosi kibovu kama timu zingine ndio maana unaona kuna timu imesajili wachezaji zaidi ya 10 hata Ulaya hilo halipo,tumekifanyia maboresho tu kikosi chetu.

“Mpaka sasa hatuna wasiwasi tuna timu bora ambayo itakapoanza kuwa sawa kila mtu ataona kazi yake,tunataka kufanya kitu kimoja cha kumalizia kutafuta beki wa kati mmoja hilo pekee ndiyo tunalolifanyia kazi sasa kulingana na benchi letu la ufundi linachotaka.

“Tulikuwa na tatizo kubwa la kiungo mkabaji na tumempata mtu ambaye hatuna mashaka naye (Papii Kabamba) atakuja nchini wakati wowote kutoka sasa kuungana na wenzake. Tutachukua na beki mmoja wa maana sana,tukimalizia huyo tutakuwa tayari kukutana na yoyote.”

Yanga inahitaji beki wa kati atakayekuwa mrithi wa Vincent Bossou aliyesaini klabu moja nchini Afrika Kusini.

Katika msimu uliopita Yanga ilionekana kuyumba katika safu ya kiungo mkabaji ambapo kukamilika kwa usajili wa Kabamba ni wazi kwamba sasa hitaji lililosalia ni kupatikana kwa beki huyo atakayesaidiana na wakongwe Kelvin Yondani,nahodha wao Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Andrew Vincent ‘Dante na ingizo jipya Abdallah Shaibu ‘Ninja’