Nyota wa Bara wakwama kujiunga Z’bar Heroes

Muktasari:

Kocha ‘Morocco’ alisema hali hiyo inatokana na viongozi wa timu hizo Yanga, Simba, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Azam, Majimaji, Prisons, Singida United pamoja na Lipuli wamegoma kuwaruhusu wachezaji wao Ligi Kuu bara itakaposimama.

Zanzibar. Kocha Mkuu timu ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’, Hemed Suleiman ‘Morocco’ amesema klabu za Tanzania bara zinamwalibia mipango yake kwa kugoma kuwaachia wachezaji wao.
Kocha ‘Morocco’ alisema hali hiyo inatokana na viongozi wa timu hizo Yanga, Simba, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Azam, Majimaji, Prisons, Singida United pamoja na Lipuli wamegoma kuwaruhusu wachezaji wao Ligi Kuu bara itakaposimama.
“Kutokana na majibu hayo ya viongozi wa timu za Tanzania bara huenda tukawasamehe hao wachezaji wanaochezea timu zao huko na kuchagua wachezaji wengine kutoka timu za hapa hapa Zanzibar ambao wataungana na wenzao katika maandalizi ya mashidano ya Cecafa”alisema Morocco.
Wachezaji waliotwaa Zanzibar Heroes kutoka klabu za bara ni pamoja na Abdallah Haji "Ninja" (Yanga), Adeyum Saleh "Machupa" (Kagera Sugar), Haji Mwinyi Ngwali (Yanga), Abdulla Kheir "Sebo" (Azam), Viungo Mudathir Yahya (Singida United), Mohd Issa "Banka" (Mtibwa Sugar) na Suleiman Kassim "Selembe" (Majimaji) pamoja na washambuliaji Kassim Suleiman (Prisons), Matteo Anton (Yanga) na Seif Rashid Abdallah “Karihe” (Lipuli).
Morocco alisema ikifika Novemba 15 ikiwa bado wachezaji hao hawajawasili katika kambi ya Heroes watalazimika kuwaacha na kuongeza nguvu kwa vijana wanaocheza klabu za Zanzibar, akidai kuwa hawawezi kuwaruhusu wachezaji hao kujiunga na kambi siku chache kabla kwenda kwenye mashindano.
Alisema uamuzi huo umekuja kutokana na timu ya taifa ya Zanzibar inatarajiwa kuondoka Novemba 22, na ligi kuu Tanzania bara inatarajiwa kwenda mapumziko Novemba 19, kwa hiyo itakuwa ni jambo gumu kwa upande wa wachezaji hao kuzoeana na wenzao kwa muda wa siku mbili au moja watakazoingia katika kambi hiyo .
 Alisema jitihada kubwa imeshafanywa na uongozi wa timu hiyo ili kuona kunafanyika mazimgumzo kati yao na viongozi wa timu za Tanzania bara ili kuona wanawapa wachezaji hao, lakini bado mazungumzo hayajaza matunda hadi wakati huu.