Yanga, Simba ubingwa bado kabisa

Muktasari:

Baada ya kuondolewa katika michuano ya Kombe la Shirikisho, akili ya Simba kwa sasa ipo Ligi Kuu Bara ikipambana kumaliza ukame wa mataji msimu huu.

KAMA wewe ni shabiki wa Simba ama Yanga na umeanza kupiga hesabu za ubingwa kwa timu yako, pole. Mpaka sasa hesabu zimekataa, iwe Msimbazi au Jangwani. Kama unabisha soma hapa.

Baada ya kuondolewa katika michuano ya Kombe la Shirikisho, akili ya Simba kwa sasa ipo Ligi Kuu Bara ikipambana kumaliza ukame wa mataji msimu huu.

Ilihali watani wao, Yanga wakiendelea na michuano ya CAF sasa wakitupwa Kombe la Shirikisho baada ya kung’olewa Ligi ya Mabingwa Afrika, nayo inapiga hesabu za kutetea taji kwa msimu wa nne mfululizo, huku ikicheza pia Kombe la FA.

Wapinzani hao wa jadi wanatoleana macho mpaka sasa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu kila moja ikiwa na alama 46, lakini Simba ikiwa na mchezo mmoja mkononi na tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Hata hivyo, bado ni mapema kutabiri nani anakwenda kubeba taji hilo msimu huu, japo tambo ni nyingi sana kwa mashabiki kwani, timu hizo zitahitaji kusafiri umbali mrefu kufuata pointi. Na hapo ndipo inakuwa ngumu upande mmoja kuanza kushangilia ndoo kwa sasa.

Yanga wamebakiwa na mechi tisa kabla ya ligi kumalizika, ambapo kati ya hizo watakipiga ugenini na Mtibwa, Mbeya City, Prisons na Mwadui.

Kuifuata Mtibwa mjini Morogoro, itasafiri kilomita 384 kwenda na kurudi.

Pia, itasafiri kilomita 822 kwenda Mbeya kukipiga mechi mbili mfululizo (Mbeya City na Prisons). Kisha iterejea Dar es Salaam ikiwa imezunguka kilomita 1,644.

Kibarua cha kusaka ubingwa nje ya Dar es Salaam kwa Yanga kitamalizia kwa safari ya Shinyanga yenye urefu wa kilomita 989 kukipiga na Mwadui kisha watarejea Dar ikiwa imekamilisha kilomita 1,978.

Kwa maana hiyo Yanga katika mechi nne ambazo itacheza ugenini, itasafiri kilomita 4,006 kwa kutumia usafiri wa anga au barabara.

Kwa upande wa Simba, imebakiwa na mechi 10 ambazo kati ya hizo tano itacheza nje ya Dar es Salaam; dhidi ya Njombe Mji (Njombe), Mtibwa (Morogoro), Lipuli (Iringa), Singida United (Singida) na Majimaji (Songea).

Simba ambayo inausaka ubingwa huo kwa nguvu msimu huu, itaanza kibarua cha kuifuata Mtibwa Morogoro ikisafiri umbali wa kilomita 384 kwenda na kurudi. Baada ya hapo watakwenda Njombe kukipiga na Njombe Mji na itasafiri umbali wa kilomita 1,420 kwenda na kurudi.

Baada ya hapo itakwenda Iringa kupambana na Lipuli ikisafiri umbali wa kilomita 984. Pia itaenda Singida kucheza na Singida United uwanjani Namfua na watasafiri umbali wa kilomita 1,392 kwenda na kurudi. Mechi ya mwisho ya ligi, Simba watakuwa Songea dhidi ya Majimaji ambapo watasafiri kwa umbali wa kilomita 1,894. Hivyo, kwa safari hiyo Simba katika mechi tano ambazo watacheza ugenini watasafiri umbali wa kilomita 6,074, wakiwazidi wapinzani wao Yanga ambao watasafiri kwa kilomita 4,006, hivyo ili kubeba ndoo yeyote kati yao itabidi kukaza msuli hasa.