Yanga, Simba kazi kwenu

VIGOGO vya soka hapa  nchini, Simba na Yanga,  zimepewa mchekea katika mechi zao za raundi ya awali za michuano ya Afrika baada ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kuwapangia timu vibonde kutoka Shelisheli na Djibout.

Hata hivyo wawakilishi hao watakuwa na kazi  ngumu wakivuka hatua hiyo kwani droo ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika watakaoshiriki mwakani inaonyesha huenda zikakutana na timu za Kiaraabu zinazowasumbua.

Yanga itakayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika itaanza na St. Louis ya Shelisheli, huku Simba itakayocheza Kombe la Shirikisho ikipangwa kuanza na Gendarmerie Nationale ya Djibout, zote zitaanzia nyumbani.

Kama Yanga itavuka katika mechi zake za kati ya Februari 9-18, itacheza na mshindi baina ya Township Rollers ya Botswana na El Merreikh ya Sudan katika mechi za raundi ya kwanza zitakazopigwa Machi9-18.

El Merreikh ni klabu anayoichezea beki kisiki, Pascal Wawa na imekuwa ikiisumbua Yanga hata katika Kombe la Kagame.

Simba inayorejea anga za kimataifa tangu mwaka 2013, ikiitoa Gendarmarie itakumbana na Al Masry ya Misri ama Green Buffaloes ya Zambia kabla ya kufuzu hatua ya play-off kuwania kuingia katika makundi.

JKU ya Zanzibar itakayocheza Ligi ya Mabingwa itaanza na Zesco United ya Zambia, huku Zimamoto ikipangiwa Welayta Dicha ya Ethiopia katika Kombe la Shirikisho Afrika.