Willian afichua dili la kuhamia Man United

London, England. Kiungo wa Brazil, Willian amesema anatamani kufanya kazi tena na Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho ambaye alimfundisha wakati akiinoa Chelsea.

Willian ambaye anahusishwa na uhamisho wa kwenda Man United, alisema Mourinho ni kati ya makocha anaotamani kufanya nao kazi siku zote.

Kiungo huyo aliyekuwa na uhakika wa namba kwenye kikosi cha Chelsea chini ya Mourinho kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu England mwaka 2015, alisema kocha huyo alimpa amani na kufurahia maisha Stamford Bridge.

Alisema Mourinho ni mtu wake wa karibu na wanaendelea kuwasiliana kwa simu na kutumiana ujumbe mfupi wa maneno.

“Natamani na ninaamini siku moja nitafanya tena kazi na Mourinho, huyu ni kati ya makocha bora wanaonivutia kutokana na kujua jukumu lao na namna alivyoishi nami wakati wote tulipokuwa Chelsea,” alisema Willian.

Hata hivyo, Willian alisema ingawa anampenda Mourinho hana maana anataka kuondoka Chelsea katika usajili wa majira ya kiangazi.

“Nia furaha hapa Chelsea ninatamani kuendelea kubaki hapa, ninapenda maisha ya jiji la London ni mji mzuri na familia yangu inapenda,”alisema nyota huyo wa Brazil.

Mchezaji huyo alisema amekataa ofa nyingi za klabu za Ulaya ikiwemo Barcelona kwa sababu anataka kubaki Chelsea msimu ujao.