Wema anakula Eid kwanza

Wema Sepetu

MALKIA wa Bongo Movies, Wema Sepetu na wafanyakazi wake wawili waokabiliwa na kesi ya kutumia dawa za kulevya katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wataanza kujitetea Juni 19, mwaka huu.

Wema na wenzake walipaswa kuanza kujitetea jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ambapo upande wa wakili wa Serikali Costantine Kakula na wakili wa utetezi Albert Msendo, wote walikuwa wapo tayari.

Lakini, ilishindikana washtakiwa hao kuanza kujitetea kwa sababu Hakimu Simba alikuwa na kazi nyingine na kesi imeahirishwa hadi Juni 19, ambapo washtakiwa wataanza kujitetea. Hatua hiyo imefikiwa baada ya Hakimu Simba kupitia ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na mashahidi watano wa upande wa mashtaka waliokuwa wakiongozwa na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula na kutoa uamuzi ambapo aliwaona washtakiwa wana kesi ya kujibu na hivyo wanapaswa kujitetea. Mbali na Wema washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ya kutumia dawa za kulevya ni Angelina Msigwa na Matrida Seleman Abbas. Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa na kutumia dawa za kulevya. Inadaiwa kuwa Februari4, 2017 katika Makazi ya Wema huko Kunduchi Ununio washtakiwa hao walikutwa na msokoto mmoja na vipisi vya bangi vya uzito wa gramu 1.08.