Wema ahukumiwa kifungo au kulipa faini Sh 2milioni

Muktasari:

Hukumu hiyo imetolewa leo, Julai 20, 2018 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya kumtia hatiani kama alivyoshatiwa.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu kulipa faini ya Sh 1Milioni kwa kila kosa au kwenda jela mwaka mmoja, baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na  kumtumia dawa za kulevya aina ya Bangi.
Hukumu hiyo imetolewa leo, Julai 20, 2018 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya kumtia hatiani kama alivyoshatiwa.
Pia, mahakama hiyo imeachia huru mshtakiwa wa pili na watatu, katika kesi hiyo, ambao ni Angelina Msigwa na Matirda Abbas.
Katika utetezi wake mahakamani hapo, Wema, alikubali kuwa nyumbani kwake palikutwa na msokoto unaodhaniwa kuwa ni bangi jikoni, vipisi ambavyo hajui nini katika chumba cha kuhifadhia nguo zake mapochi na viatu na kiberiti katika chumba wanacholala wanamuziki wawili Jodarn na Mila.
Akiongozwa na wakili Msando kujitetea, Wema alieleza kuwa yeye hajui vitu hivyo ni vyanani  kwa sababu yeye ni msanii wa filamu na nyumbani kwake wanaingia watu tofauti tofauti pia huwa anafanya pati na kualika watu katika nyama choma na chakula cha mchana.
Hivyo hawezi kujua vitu hivyo ni vya nani na kwamba watu wengine huwa wanaingia jikoni kwake na maeneo mengine isipokuwa katika chumba chake cha kulala kwa kuwa huwa anafunga.
Wema alidai kuwa polisi walikagua katika chumba chake cha kulala, lakini hawakupata kitu.
Alibainisha kuwa nyumbani kwake walikuwa wanaishi yeye, wafanyakazi wake wawili, wadogo zake wawili,  Agray Philemon na Fanuel Evalast na vijana wawilï wanamuziki Milaji na Jordan.
Alidai kuwa Februari 3, 2017 aliitwa polisi wakaripoti polisi kati saa tano asubuhi kwa idhinï ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda.
"Siku hiyo tulifika polisi saa tano asubuhi na wenzangu watano tukasubiri hadi saa 10 jioni, ulipofika muda huo alifika Makonda na kutuita mmoja mmoja katika chumba ambapo alikuwepo na Afande Siro" Alieleza Wema.
Alidai kuwa wakiwa humo aliulizwa kama anatumia dawa ya kulevya ama kuuza  na kwamba aliwajibu hapana.
Aliendelea kudai kuwa baada ya mahojiano hayo walpelekwa mahabusu ambapo walikaa kwa siku saba na kwamba kati ya siku hizo, Februari 5, 2017 Jumapili polisi, akiwamo afande Mery, OCCID Denis, Hassani walimpeleka kwake kufanya upekuzi.
Wema alibainisha kuwa wakiwa njiani hawakuongea chochote na afande Mery safari yote walikuwa kimya tu.
Wema aliongeza kuwa yeye alitoa sampuli ya mkojo polisi na kwamba alimkabidhi afande Mery na kwamba yeye hana lolote la kueleza mahakama.
Inadaiwa kuwa Februari 4, 2017 katika Makazi ya Wema huko Kunduchi Ununio  washtakiwa hao walikutwa na msokoto mmoja na vipisi vya bangi vyenye uzito wa gramu 1.08.
Kwa upande wa Wema yeye anadaiwa kuwa Februari Mosi, 2017 katika  eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam, alitumia dawa za kulevya aina ya Bangi.