Wema ahepa jela, alipa faini

Muktasari:

Wema amelipa faini hiyo baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana Ijumaa kumhukumu kwenda jela mwaka mmoja ama kulipa faini hiyo kwa kila kosa baada ya kutiwa hatiani kwa mashitaka ya kukutwa na kutumia dawa za kulevya aina ya bangi.

MALKIA wa Bongo Movie, Wema Sepetu, amenusuruka kwenda jela mwaka mmoja baada ya kulipa faini ya Sh2 milioni.

Wema amelipa faini hiyo baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana Ijumaa kumhukumu kwenda jela mwaka mmoja ama kulipa faini hiyo kwa kila kosa baada ya kutiwa hatiani kwa mashitaka ya kukutwa na kutumia dawa za kulevya aina ya bangi.

Wakati Wema akikutwa na hatia, washitakiwa wenzake katika kesi hiyo ambao ni wafanyakazi wake wa ndani; Angelina Msigwa na Matrida Abbas, wameachiwa huru baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao.

Akisoma hukumu hiyo iliyochukua zaidi ya dakika 45, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, alisema upande wa mashitaka ulileta mashahidi watano ambao walithibitisha mashitaka hayo.

Hakimu huyo alisema baada ya upande wa mashitaka kufunga ushahidi wake, washitakiwa wote walikutwa na kesi ya kujibu na walijitetea wakiongozwa na Wakili Albert Msando.

“Unajua ni jukumu la upande wa mashitaka kuthibitisha mashitaka bila ya kuacha shaka na si mshitakiwa,” alisema Hakimu Simba na kuongeza kusema: “Pia upande wa mashtaka unapaswa kuthibitisha kuwa Wema anatumia dawa za kulevya pasina kuacha shaka yoyote.”

Aliendelea kusema kuwa, mshitakiwa wa pili na wa tatu hawakushiriki kwenye upekuzi katika nyumba ya Wema na bangi zilikutwa jikoni, chumbani na kwenye kiberiti, ndani ya nyumba ya Wema.

Alieleza kuwa mshitakiwa mwenyewe katika ushahidi wake alikiri kukutwa na bangi nyumbani kwake, alitia saini katika barua ya upekuzi na alikubali mkojo wake uliochukuliwa na kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.

“Nawaachia huru mshitakiwa wa pili na wa tatu kwa kuwa upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao, lakini kwa upande wa Wema hakuna shaka yoyote kwamba, alipatikana na dawa za kulevya” alisema Hakimu.

Hali ilivyokuwa Mahakamani

Mashabiki wa Wema walifurika katika mahakama hiyo kusikiliza hukumu huku wakionekana kuwa na wasiwasi.

Mbali ya mashabiki hao, mama yake Wema, Miriam Sepetu, Meneja wake Martine Kadinda na dada yake, ni miongoni mwa watu waliohudhuria kesi hiyo na muda wote walikuwa na nyuso za upole, tofauti na siku nyingine.

Kwa upande wake Wema, ambaye jana hakujiremba, alifika mahakamani hapo asubuhi na kukaa kwenye gari hadi muda wa kesi ulipofika ndio alipoingia katika chumba cha mahakama akiambatana na mama yake, lakini wakati huo hakuonyesha nyuso ya furaha kama ilivyo siku nyingine.

Hata alipopanda kizimbani wakati hukumu hiyo inasomwa, Wema alitumia muda mwingi kuinamisha kichwa.