Wellington Ochieng kuongeza nguvu Gor Mahia dhidi ya Simba

Muktasari:

  • Hizi ni habari mbaya kwa wapinzani wa Kogalo, mabingwa wa soka Tanzania Bara, Klabu ya Simba SC, hasa ukizingatia ubutu wa safu ya ushambuliaji ya kikosi chao maarufu kwa jina la Wekundu wa Msimbazi, ambao hawajafanikiwa kufunga bao lolote ndani ya dakika 90, katika michuano hiyo.

Nairobi, Ikiwa imesalia masaa machache kabla ya mtanange wa kukata na shoka wa fainali ya  pili ya SportPesa Super Cup, morali imeongezeka katika kambi ya mabingwa watetezi Gor Mahia, baada ya beki wake kisiki, Wellington Ochieng kurejea.
Hizi ni habari mbaya kwa wapinzani wa Kogalo, mabingwa wa soka Tanzania Bara, Klabu ya Simba SC, hasa ukizingatia ubutu wa safu ya ushambuliaji ya kikosi chao maarufu kwa jina la Wekundu wa Msimbazi, ambao hawajafanikiwa kufunga bao lolote ndani ya dakika 90, katika michuano hiyo.
Beki huyo wa kulia, amekuwa nje kwa takribani miezi minne akiuguza jeraha la goti na kwa mujibu wa taarifa zilizoifikia Mwanaspoti Digital ni kwamba, beki huyo yuko tayari kuwavaa Simba katika mechi ya fainali, itakayopigwa kesho kuanzia saa 9 alasiri, Uwanja wa Afraha.
Klabu ya Gor Mahia imethibitisha kuwa, nyota huyo wa zamani wa Muhoroni Youth, atakuwepo katika kikosi cha Kocha, Mwingereza Dylan Kerr kesho na tayari ameshajiunga na timu mjini Nakuru na wamesisitiza uwepo wake utaongeza morali kwao.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu hiyo, Wellington ambaye nafasi yake, ilikuwa inajazwa na Philemon Otieno na Innocent Wafula, amesema anafurahia kuungana na wenzake huku akiwatahadharisha Simba wajiandae kwa shughuli pevu.
“Nimefarijika sana kurejea kikosini. Niko fiti na tayari kuendeleza mapambano. Kwa sasa namsikiliza Kocha, kama atanipa nafasi kesho, nitashukuru sana na naahidi kufanya kazi yangu, Simba wajiandae," amesema Ochieng.
Gor Mahia walijikatia tiketi ya kwenda fainali kwa kuifungisha virago Klabu ya Singida United, kwa ushindi wa mabao 2-0, katika mechi ya nusu fainali ya pili. Kwa upande wao Simba walifuzu kwa kuiong'oa Kakamega Homeboyz kwa mikwaju ya penalti 5-4.
Mshindi wa makala ya pili ya SportPesa Super Cup, ataondoka na kitita cha shilingi milioni 3 (sawa na Tsh60 milioni), Kombe na fursa ya kwenda Goodison Park, nchini Uingereza kucheza na Everton FC.