Wawa bwana kumbe anajua kila kitu!

Muktasari:

  • Klabu za Simba na Yanga zimeonyesha nia ya kumuhitaji mchezaji huyo mwenye historia kwenye michuano ya Kombe la Kagame baada ya kuwa mchezaji bora mara tano.

Dar es Salaam. Beki Muivory Coast anayewaniwa na Simba na Yanga, Pascal Wawa, anafuatilia na anajua kila kitu kinachoendelea Bongo na hasa mpango wake wa usajili, kisha akasema yote anamwachia Mungu.

Wawa ambaye kwa sasa yupo kwao Ivory Coast, anajifua vilivyo na timu yake ya zamani ya academi kuona anakuwa vizuri wakati wote.

Si unajua mambo ya mtandao katika miaka hii, anazo picha za magazeti yote yanayotoa habari zake, anafuatilia mitandao yote ya kijamii kama Istagram.

Na akasema: "Najua kila kitu kinachoendelea huko, kwa upande wangu, suala hili nimeamua kumwachia Mungu."

Alipouliza kwa nini anamwachia Mungu amesema: "Kama hivyo timu zinanitafuta lakini mwisho wa siku inabidi jambo likamilike na katika yote hayo, Mungu ndiye anayejua."

Wawa ni maarufu nchini kutokana na namna alivyofanya vizuri katika mashindano tofauti ndani ya kikosi cha Azam FC.