Washambuliaji Alliance wamkuna Makata

Muktasari:

Washambuliaji Chinedu Nwankwoeze na Wayyeka Tatuwe kila mmoja alifunga bao katika ushindi wao wa mabao 2-1 dhidi Kagera Sugar katika mchezo wa kirafiki uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Nyamagana.

Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Alliance, Mbwana Makata amewasifia washambuliaji wake wa kigeni na kuwataka kuendeleza makali hayo katika Ligi Kuu inayotarajia kuanza Agosti 22 mwaka huu.

Washambuliaji Chinedu Nwankwoeze na Wayyeka Tatuwe kila mmoja alifunga bao katika ushindi wao wa mabao 2-1 dhidi Kagera Sugar katika mchezo wa kirafiki uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Nyamagana.

Makata alisema mbali na kufanikiwa kuibuka na ushindi huo bado kuna tatizo katika suala la kasi ya uchezaji na kuweka wazi pia safu yake ya ushambuliaji inakosa umakini kwa sababu ilitengeneza nafasi nyingi, lakini ilitumia mbili tu.

Alisema Kagera Sugar ni kipimo sahihi kwa timu yake kutokana na timu hiyo kuwa na uzoefu katika ligi na anaamini mchezo huo umewajenga kisaikolojia wachezaji wake ambao hawajawahi kushiriki Ligi.

"Siwezi kuridhika na matokeo hayo na nikabweteka nitaendelea kupambana kuhakikisha kikosi changu kinakuwa imara zaidi pia natarajia kuyafanyia kazi makosa yaliyojitokeza katika mchezo huo hasa katika safu ya ushambuliaji kwa sababu naamini mabao pia ndiyo yanayoamua ubingwa au timu kushuka daraja."

Makata aliongeza kikosi chake kimeanza kuzoeana kutokana na michezo hiyo waliyocheza hadi sasa.