Wanavaa viatu vya Yondani Jangwani

Dirisha la usajili wa Ligi Kuu Bara lilifungwa mwishoni mwa Julai na kabla ya kufungwa kwake, mabosi wa Yanga walihenyeka sana kumzuia beki wao wa nguvu, Kelvin Yondani asiondoke.

Beki huyo wa kati wa Yanga na Taifa Stars alitaka awekewe mezani mzigo wa maana ndipo adondoke saini na kusababisha mabosi wa timu hiyo kuhaha ni vipi watamalizana naye kabla ya dakika za mwisho kufanikiwa kumtuliza klabuni hapo.

Hata hivyo, hakuna ajuaye nini kilifanyika na filamu hii inaweza ikaendelea kipindi cha usajili wa dirisha dogo au lile la baada ya msimu iwapo tu mzigo waliokubaliana utakuwa haujatimizwa.

Achana na hayo ya usajili. Ishu nzima ni kuhusu nani atamrithi pale Jangwani?

Hakuna asiyejua uwezo wa Yondani Yanga na soka la Tanzania kwa jumla. Ni beki wa shughuli na kila kocha makini angependa kuwa naye katika kikosi chake

Hata hivyo, kila jambo lina mwisho wake. Wachezaji wengi waliotamba miaka ya nyuma si hapa tu Bongo, hata duniani kwa jumla, wameshatundika daruga na kuacha sifa kemkem.

Hata juzi kati tu, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alitangaza kustaafu soka na ameacha ifa kemkem. Ni wazi uwezo wake ulifika mwisho na sasa anahitaji kuwaachia wengine.

Itakuwa hivyo kwa mchezaji yeyote na hata Yandani ambaye kwa sasa anahesabika kati ya mabeki bora zaidi wa kati nchini.

Hata hivyo, kama tu ataamua kupumzika ni nani ataweza kuvaa viatu vyake?

Pale Jangwani kwa sasa, kuna mtu anaitwa, Andrew Vincent ‘Dante’ anayeonekana kuziba nafasi ya Cannavaro, huku Abdallah Shaibu ‘Ninja’, akionekana bado anahitaji muda zaidi wa kuhimili vishindo vya beki ya kati ndani ya Yanga.

Hata hivyo, Mwanaspoti limewamulika baadhi ya mabeki ambao kutokana na ukomavu wao wanaweza kuwa warithi sahihi wa Yondani ndani ya Yanga kama ambavyo Dante alivyoandaliwa kumrithi Cannavaro.

ABDALLAH MFUKO

Beki huyu alianzia maisha yake ya soka kiushindani Coastal Union ya Tanga na ukomavu wake ulisababisha timu nyingi kupigana vikumbo kuitaka saini yake.

Ilikuwa hivyo kwa Simba, lakini mwishowe aliibukia Mwadui akiwa katika kiwango kizuri misimu miwili mfululizo tangu timu hiyo ikiwa chini ya Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na sasa Mnyarwanda Ally Bizimungu na msimu ujao atakuwa na Ndanda FC.

Hata hivyo, beki huyu mwenye umbo kubwa na misuli iliyotanuka amekuwa chachu kwa washambuliaji wa timu pinzani na kutokana na ufiti alio nao na uzoefu wa kutosha Ligi Kuu, anaweza kabisa kurithi viatu vya Yondani pale Yanga na mashabiki wakaamini Yondani bado yuko Jangwani kutakana na aina ya uchezaji wao.

ABDALLAH KHERI ‘SEBO’

Sio beki mwenye makeke hata kidogo anapokuwa kazini, lakini ni mmoja ya mabeki wanaocheza kama Yondani ama Cannavaro ndani ya kikosi cha Azam FC.

Katika michuano ya Kombe la Kagame aliunda safu nzuri ya ulinzi akiwa sambamba na mkongwe Aggery Morris.

Alikuwa hapati nafasi mbele ya Yakub Mohammed, ila tangu Mghana huyo alipoumia msimu uliopita, Sebo alipata nafasi ya kucheza na hakufanya makosa.

Akili na nguvu alizonazo aliweza kutulia na kuifanya kazi yake vizuri, pia ana umbo ambalo linamruhusu kupambana na mshambuliaji wa aina yoyote.

Anaweza kuwa mrithi sahihi wa Yondani kwa vile licha ya kuwa na umri mdogo, lakini ameonyesha ukomavu akiwa Azam ndanio ya Ligi mpaka kuisaidia timu yao kutetea Kombe la Kagame.

PAUL BUKABA

Katika nafasi ya beki wa kati hivi sasa yakikosi cha Simba inawezekana kabisa kutakuwa na ushindani mkubwa, hili linatokana na idadi na aina ya wachezaji wanaocheza nafasi hiyo.

Bukaba alikuwa hapati nafasi ya kuanza Simba msimu uliopita, lakini alipopewa nafasi Kombe la Kagame alionyesha kiwango kikubwa na utulivu akisaidiana na Serge Pascal Wawa.

Ana uwezo mkubwa wa kutulia na mpira, nguvu na akili ya kujilinda, umri wake bado ni mdogo, lakini utayari wake katika ushindani ni mkubwa sana wa kucheza kikosi chochote.

Bila shaka kama Yanga wanaweza kumfikiria mchezaji wa haraka wa kuziba nafasi ya Yondani, basi ni huyu Bukaba kwani ukimtazama kwa jicho la karibu utagundua ndani yake kuna Yondani mwingine aliyevaa jezi ya Msimbazi.

MOHAMMED FAKHI

Akiwa hajavaa jezi anatembea mtaani unaweza ukasema ni bishoo mmoja ambaye anajaribu kucheza mpira, lakini unapomwona ndani ya dakika kumi uwanjani basi utapata kitu unachotaka kufahamu kutoka kwake.

Fakhi, aliyewahi kuichezea Simba ikimtoa JKT Ruvu na walivutiwa na huduma yake, lakini licha ya uwezo wake ilimchukua muda kupata nafasi katika kikosi hicho na ndipo alipoamua kujiunga na Kagera Sugar.

Akiwa na Kagera Sugar akicheza pamoja na Juma Nyosso ndipo kila mmoja alipoanza kuona uwezo wake na hadi kufikia hatua ya kupewa kitambaa cha unahodha katika timu hiyo ,benchi la ufundi walikuwa wameona mengi.

Amejiunga na JKT Tanzania lakini bado Yanga kama inahitaji mtu sahihi wa kuchukua nafasi ya Yondani badi Fakhi anawafaa, muhimu tu asiendelee na tatizo lake la kupata majeraha ya mara kwa mara.

KULWA IDD MOBBY

Ukiitaja Mwadui FC, lazima tu utaanza kulifikiria jina hili kisha ndio yatafuata mengine kama ya Paul Nonga.

Mobby ni beki katili katika kikosi cha Mwadui na uwezo wake umemfanya awe tishio katika kikosi hicho.

Alikuwa pacha mzuri akisaidiana na Abdallah Mfuko katika kikosi hicho na ulitakiwa upambane hasa ili tu uweze kupenya katika kumi na nane yao, kwani walikuwa na mawasiliano ya kutosha katika kikosi hicho pindi wanapocheza pamoja.

Mobby aliwahi kuitajika na Simba lakini ilitajwa dau alilokuwa amewekewa kipindi hicho ndio lilimfanya aendelee kusalia katika kikosi hicho cha Mwadui.

Bila shaka anaweza kuwa miongoni mwa mabeki wanaoweza kurithi mikoba ya Yondani katika kikosi cha Yanga, kwa sababu tayari ana uzoefu na ligi na ameshapambana na washambuliaji tofauti katika ligi hiyo inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 22.