Wanasoka matajiri wenye umri mdogo huko Ulaya

Muktasari:

Wapo wachezaji wachache wenye umri kuanzia miaka 26 na kushuka chini ndiyo matajiri, wakivuna pesa za kutosha kutokana na kazi yao hiyo ya kusakata soka.

LONDONENGLAND.

KWA wanasoka matajiri zaidi duniani, wengi wake wamevuka umri wa miaka 30. Na wale waliochini ya miaka 30, wengi wao wana umri wa kati ya miaka 27 na 29.

Wapo wachezaji wachache wenye umri kuanzia miaka 26 na kushuka chini ndiyo matajiri, wakivuna pesa za kutosha kutokana na kazi yao hiyo ya kusakata soka.

Makala haya yanawahusu wachezaji watano matajiri wenye umri mdogo kuanzia miaka 26 kushuka chini, ambao wanatamba kwenye soka la Ulaya kwa sasa.

5. David Alaba, Dola 20 milioni

David Alaba ni mmoja kati ya wachezaji mahiri kabisa waliolishika soka la Ulaya. Huduma yake anayotoa huko Bayern Munich anahesabika kama beki wa kushoto, lakini anapokwenda kwenye timu yake ya Taifa ya Austria, anahesabika kama kiungo mshambuliaji, wakati mwingine anacheza kama kiungo wa kati. Aliwahi pia kuichezea Hoffenheim.

Akiwa na umri wa miaka 25 tu, Alaba ametengeneza pesa zinazomfanya kuwa mchezaji tajiri kijana kutokana na kuwa na kipato cha Dola 20 milioni. Ana dili pia za kibiashara na kampuni kama ya Adidas na hivyo kupiga pesa tu zinazomfanya aendelee kuwatesa vijana wenzake kutokana na kipato chake.

4. Romelu Lukaku, Dola 20 milioni

Mwili jumba, lakini umri wa Romelu Lukaku ni miaka 24 tu. Kwa maana hiyo bado ni mchezaji kijana, anayehitaji muda mrefu zaidi wa kucheza na kwenda kuwa mshambuliaji mwenye uzoefu mkubwa katika mchezo huo wa soka. Kwa sasa ni mshambuliaji wa Manchester United na mshahara wake anaolipwa huko umemfanya kuzidi kuwa na utajiri zaidi baada ya kuripotiwa kwa sasa kuwa na kipato cha Dola 20 milioni. Kwa takwimu za kipesa zilizoripotiwa siku za karibuni ni kwamba utajiri wa Lukaku unaweza kuongezeka kwa asilimia 23 ndani ya kipindi kifupi kijacho na hicho kumfanya aendelee kuwa mchezaji kijana tajiri.Kipato cha Dola 20 milioni si kitoto.

3. Mario Gotze, Dola 35 milioni

Mjerumani Mario Gotze ana miaka 25 tu, lakini ni miongoni mwa wanasoka vijana wanaopiga pesa na kuwa matajiri.

Kipato cha staa huyo anayekipiga katika kikosi cha Borussia Dortmund kimeripotiwa kuwa Dola 35 milioni. Gotze anaichezea pia Timu ya Taifa ya Ujerumani. Ukiweka kando mishahara anayovuna kwenye soka ambapo aliwahi pia kuichezea Bayern Munich, Gotze anapiga pesa pia kupitia dili mbalimbali za kibiashara kama vile Nike, Konami na Samsung. Madili kama hayo ndiyo yanayomfanya Gotze kuwa kwenye orodha ya wachezaji vijana wanaopiga pesa ndefu kutokana na kuwa na utajiri wa Dola 35 milioni.

2. Paul Pogba, Dola 60 milioni

Kwa miaka mitatu ijayo, utajiri wa Pogba utaongezeka kwa asilimia 130 na hivyo kumfanya awe na pesa ndefu zaidi. Staa huyo wa Manchester United, hivi karibuni tu alitimiza umri wa miaka 25, lakini linapokuja suala la mkwanja, kiungo huyo yupo vizuri. Pogba anaripotiwa kuwa na kipato cha Dola 60 milioni. Kuwa na kiwango bora kwenye soka na limemfanya kuwa kivutio kikubwa kwa makampuni ya kibiashara na kuzidi kujitengenezea pesa ya kutosha zaidi. Kwa umri aliokuwa nao kisha kuwa na kipato cha Dola 60 milioni si jambo dogo na ndiyo maana staa huyo amekuwa na vurugu nyingi nje ya uwanja akiwatambua vijana wenzake.

1. Neymar, Dola 140 milioni

Supastaa wa Kibrazili, Neymar umri wake ni miaka 26 tu, lakini pesa anayomiliki si mchezo. Staa huyo nayekipiga Paris Saint-Germain, amedaiwa kuwa na kipato cha Dola 140 milioni.

Mshahara wa Neymar umezidi kumfanya kuwa tajiri mdogo kwa sababu ni mmoja kati ya wachezaji wanaolipwa pesa nzuri zaidi duniani. Jarida la Forbes limeripoti Neymar alivuna Dola 22 milioni mwaka 2016.

Neymar ana dili nyingine pia za kibiashara kama vile Nike, Gillette, Beats Electronics na Red Bull, ambazo zimemwingiza Pauni 2.7 milioni kila mwezi, sawa na Pauni 600,000 kwa wiki, au Pauni 4000 kwa sasa kwa hesabu zisizo rasmi sana.