Wanariadha waagwa Arusha, wahidi kufanya vyema mashindano ya dunia

Tuesday July 11 2017

By Yohana Challe, Mwananchi

Arusha: Wanariadha wawili wa Tanzania Winfrida Makenji na Shomari Mtauni, wameagwa mkoani hapa leo Jumanne tayari kwa safari ya Kenya kwenda katika mashindano ya Riadha ya Vijana ya Dunia yanayotarajia kuanza kufanyika kesho Jumatano nchini humo.

Mwanariadha Winfrida amehaidi kufanya vizuri katika mbio anazoshiriki za mita 100 na 200 huku akiomba dua kwa Watanzania ili awe na afya nzuri wakati wa mashindano hayo.

Naye Shomari alioomba RT na Serikali kuwaunga mkono wanariadha kwa sababu waliofuzu michuano hiyo walikuwa 12 na muda wote walikuwa kambini Kibaha wakijinoa tayari kwa michuano, lakini kutokana na ukata wanariadha wawili ndio waliosafirishwa.

Wanariadha hao wameambatana na kocha wa timu hiyo Rehema Kilo sambamba na Christian Matembo ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya nidhamu na usuluhishi ya shirikisho la riadha nchini (RT).

Mashindano hayo ya dunia yatafanyika kwa siku tano kuanzia kesho, Jumatano Julai 12 hadi Julai 16, kwa nchi zaidi 200 Duniani  wanachama wa shirikisho la riadha Duniani (IAAF).