Wanariadha wa Madola wapigwa panga

Arusha. Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) linatarajia kukutana Juni 9 kuwajadili wanariadha walioonesha nidhamu mbovu baada ya kurejea nchini kutoka Australia walipokwenda kushiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika Mjini Gold Coast.
Katibu Mkuu wa RT Wilhelm Gidabuday alisema kuwa kamati tendaji itakutana siku hiyo ikiwa na ajenda tano nyingine zikiwa ni kujua tarehe ya mashindano ya riadha ya Taifa ambayo mwaka jana hayakufanyika kutokana na maandalizi ya mashindano ya Dunia waliyokuwa wakifanya.
“Baada ya wanariadha kurejea nchini tulipokea taarifa za viongozi wao lakini hatukupata muda wa kamati tendaji kukaa na kujadili na sasa ni muda mwafaka umewadia ili kujua mustakabali wa mchezo wa riadha,” alisema Gidabuday.
Pamoja na hilo ajenda nyingine itakuwa ni juu ya maandalizi ya mashindano ya kanda yatakayofanyika mwishoni mwa mwezi ujao wakati nchi 11 zitakapooneshana ubavu wa kufukuza upepo jijini Dar es Salaam.
Gidabuday aliongeza kuwa watakuwa na kazi ya kupitia katiba ya RT ili kuhakikisha wanaenda kwa kasi  kuelekea mashindano makubwa yanayowakabili kuanzia mwaka huu hadi mwaka 2020 kwenye michuano ya Olimpiki.
Wanariadha waliokwenda kupeperusha bendera ya Tanzania huko Australia alikuwa Said Makula, Stephano Huche, Sarah Ramadhanm Failuna Abdi, Hamis Gullam na Anthony Mwanga.