Wametoswa tu Ila Wanafaa Kuwania Tuzo Bora ya Ubora EPL

Muktasari:

  • Kuna mastaa sita, Kevin De Bruyne, Mohamed Salah, David De Gea, David Silva, Leroy Sane na Harry Kane.

ISHU ya nani atakuwa mchezaji bora wa mwaka kwenye Ligi Kuu England msimu huu, imeshafahamika na haiwezi kuwa nje ya wachezaji sita waliotangazwa kuwania tuzo hiyo kwa sasa.

Kuna mastaa sita, Kevin De Bruyne, Mohamed Salah, David De Gea, David Silva, Leroy Sane na Harry Kane.

Hata hivyo, kwenye orodha hiyo, majina mawili yanapewa nafasi kubwa kuwa ndio watakaokuwa washindani wa kweli ambao ni De Bruyne na Mo Salah na hao wengine kwa maana hiyo ni wa kusindikiza tu washindi.

Katika kuingia kwenye orodha hiyo, kila mmoja ana kigezo chake na hicho ndicho kinachoweza kutoa tathmini ya ubora wa kila mchezaji kwa msimu husika.

Hakuna ubishi wowote kuwa wakali hao sita hakuna asiyestahili kuwamo kwenye orodha ya wanaoshindania tuzo hiyo, lakini isingekuwa shida tena kama moja ya majina ya mastaa hawa lingekuwapo kwenye orodha hiyo.

Hawa hapa wakali watano ambao wamekuwa bora kabisa katika Ligi Kuu England msimu huu na isingekuwa shida kama majina yao yangejumuishwa kwenye yale ya kuwania tuzo ya kumtafuta mchezaji bora wa mwaka wa ligi hiyo.

1.Christian Eriksen (Tottenham)

Kama kuna mafundi wa mpira waliopata kutokea Ligi Kuu England, basi kuwapo kwa staa wa kimataifa wa Denmark, Christian Eriksen huko Tottenham Hotspur.

Eriksen ni fundi wa mpira na anapokuwa uwanjani siku zote pasi zake zimekuwa na macho na kuwafikia walengwa kwa wakati mwafaka.

Kiungo huyo mchezeshaji ni aina ya mchezaji ambaye yeye ndiye anayeamua timu icheze na adui achezeje kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa nao katika kuumiliki mchezo anavyotaka yeye.

Kama unamzungumzia De Bruyne kuwa bora msimu huu, basi huwezi kumweka mbali Eriksen kutokana na mchango wake kwa Spurs.

Eriksen amefunga mabao 10 na kuasisti mengine tisa na kumfanya awe kwenye orodha ya wakali 10 waliopiga asisti nyingi kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

2. Roberto Firmino (Liverpool)

Kwenye kikosi cha Liverpool msimu huu huwambii kitu kuhusu Mohamed Salah. Staa huyo anacheza soka la ubora wake na kufunga kwa kadiri anavyotaka. Lakini kwenye kikosi hicho kuna staa huyo anayefanya kazi kubwa sana inayoifanya safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho cha Kocha Jurgen Klopp kuwa tishio ni Roberto Firmino.

Kocha Klopp ameshawahi kumzungumzia staa huyo wa Kibrazili kuwa anakupa unachokitaka ndani ya uwanja.

Kwenye Ligi Kuu, Firmino amefunga mabao 15 na kuasisti mengine saba, hivyo kukifanya kikosi cha Liverpool kuendelea na mapambano ya kuhakikisha kinamaliza ligi ndani ya Top Four ili kunyakua tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

3.Raheem Sterling

(Man City)

Huenda Pep Guardiola asipate fursa ya kumfundisha mchezaji mwenye uwezo mkubwa kama wa Lionel Messi katika maisha yake yote ya ukocha, lakini kuna wale wachezaji wanaofahamu vyema maelezo yake ya ndani ya uwanja na mmoja wao ni Raheem Sterling huko kwenye kikosi cha Manchester City.

Guardiola amemfanya Sterling kuwa Messi wa Man City baada ya kumtumia kama namba 9 kivuli, eneo ambalo limemsaidia Mwingereza huyo kuboresha kiwango chake cha kupasia mipira wavuni.

Sterling wa Guardiola ameonekana kupevuka kwelikweli licha ya kuonekana kama kuna kitu hakipo vizuri kwenye umaliziaji wake.

Hata hivyo, ametikisa mabao 17 kwenye Ligi Kuu England na kuasisti mara nane, si haba.

4.Nick Pope (Burnley)

Kama kuna kitu kinampasua kichwa Sean Dyche kwenye kikosi chake cha Burnley, basi ni uamuzi wa kipa gani wa kubaki naye kwa ajili ya msimu ujao kati ya Tom Heaton na Nick Pope.

Hakika Nick Pope amekuwa kwenye kwiango kizuri kabisa msimu huu na hicho ndicho kinachoifanya Burnley kuwa matokeo mazuri kwa msimu huu kwa sababu golini hawajaweka shati.

Kwenye ligi msimu huu, Burnley inashika namba tatu wa kuruhusu mabao machache na hilo linatokana na huduma bora kabisa kutoka kwa kipa wake, hasa namna mbili, Nick Pope, aliyeokoa hatari 100 zilizoonekana kuwa mabao.

5.Nemanja Matic (Man United)

Hii ni mara kwanza, Jose Mourinho, ameshindwa kubeba ubingwa wa ligi kwenye msimu wake wa pili katika klabu anayoifundisha.

Ndiyo maana hiki kimekuwa kipindi kigumu zaidi kwa Mourinho.

Kwa msimu huu, Mourinho itabidi akubali tu na apambane na hali yake kuhakikisha kikosi chake cha Manchester United kinamaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Katika moja ya watumishi bora wa Mourinho kwa msimu huu kwenye Ligi Kuu England ni Nemanja Matic, ambaye alisaidia kwenye kuilinda Man United isifungwe mabao ya kizembe, akinasa mipira njiani mara 59 na kupora kutoka kwenye miguu ya wachezaji wengine mara 65.