Wambura ana nafasi ya kuibuka shujaa au kuzama

MWAKA 2000 tukiwa tumemaliza kucheza mechi ya soka ya waandishi wa habari viwanja vya Leaders Club, alikuja aliyekuwa Katibu Mkuu wa FAT (sasa TFF), Ismail Aden Rage.

Rage alichukua mpira akapiga danadana mbili tatu kisha akaupiga juu na kuuchezea kwa kichwa mara nne au tano halafu akasema: “Mwambieni…. (akamtaja jina kiongozi aliyemtangulia FAT) naye aje afanye hivyo kama ataweza.”

Baadaye gazeti moja lilichora katuni ya Rage iliyolielezea tukio lile na kuongeza maneno yafuatayo, “Rage kumbe wamo.” Katuni hiyo pia ilikuwa na ufafanuzi uliosomeka: “Haikuweza kufahamika mara moja kwa nini Rage alimtaja jina kiongozi huyo baada ya kuonyesha ufundi wa kuuchezea mpira.” Wakati baadhi ya waandishi wakijiuliza kulikoni Rage kumtaja kiongozi huyo, mwandishi mmoja mkongwe wa wakati huo alisema aliyemtaja ni mpinzani wake katika Uchaguzi Mkuu wa FAT mwaka 2001.

Mwandishi mwingine ambaye pia ni mkongwe kwa wakati huo, alisema kama Rage anafikiri mpinzani wake ni huyo tu atakuwa amekosea, mpinzani wake mwingine ni Michael Richard Wambura ambaye ana nguvu na anaweza kumshangaza.

Miaka mingi imepita, lakini maneno haya bado nayakumbuka hasa kwa kuwa ndicho kilichotokea katika uchaguzi uliofanyika mkoani Arusha, Wambura alimbwaga Rage. Katika kipindi cha uongozi wa Rage na Mwenyekiti wake Muhidini Ndolanga, soka la Tanzania liliandamwa na migogoro hasa ile ya klabu za Simba na Yanga pamoja na ugomvi wa ndani kwa ndani baina ya viongozi wa FAT.

Alipoingia Wambura migogoro ya ndani ya FAT, ikachukua sura mpya, akawa vitani na mwenyekiti wake Ndolanga, ilikuwa vita iliyotawala soka la Tanzania.

Kwa mtazamo wangu kama kuna wakati soka la Tanzania lilipitia kipindi cha migogoro ya ajabu ajabu basi ni wakati wa utawala wa Wambura na Ndolanga. Ilikuwa hajulikani nani bosi kwa mwenzake. Ilifikia wakati hata ratiba za ligi zilikuwa hazieleweki, nakumbuka kuna siku mechi ya ligi ilipangwa kuchezwa Uwanja wa Uhuru, lakini wamiliki wa uwanja wakaufunga kuzuia mechi isichezwe kwa makosa ambayo wamiliki walidai yalianzia FAT.

Kulikuwa na matukio mengi ya ajabu ajabu ikiwamo soka kuchezwa mahakamani na mkutano mkuu wa FAT kujadili migogoro zaidi kuliko maendeleo.

Migogoro au minyukano isiyo na mbele wala nyuma ilikoma au kupungua kwa kiasi kikubwa baada ya uchaguzi wa Desemba 2004 uliomwingiza madarakani Leodegar Tenga na timu mpya huku FAT ikibadilishwa jina na kuwa TFF. Si katika TFF tu bali hata Simba na Yanga nako hali ilitulia kwa kiasi kikubwa.

Wakati aliyekuwa mpinzani wa Wambura, Rage akifanikiwa kurudi TFF katika uchaguzi uliofuata akiwa Makamu wa Pili wa Rais, kwa Wambura nafasi hiyo hakuweza kuipata licha ya kuipigania.

Kila alipochomoza kuwania nafasi ya uongozi ndani ya TFF iwe mkoani au Taifa alikumbana na vikwazo vya kila aina zikiwamo hoja za matumizi mabaya ya ofisi. Alipambana kutaka kuwania uongozi uchaguzi wa 2008/09 lakini jina lake lilikatwa.

Kwa vikwazo alivyokutana navyo ilifikia wakati baadhi yetu tukaona kama kulikuwa na mkakati maalumu kumdhibiti Wambura kuongoza soka la Tanzania.Kitendo cha Wambura kushinda uchaguzi wa Agosti 2017 na kurejea uongozi wa juu wa TFF ilikuwa ushindi mkubwa kwake na kwa watu wake wa karibu, ilionyesha jinsi alivyo mpiganaji asiyechoka wala kukata tamaa, kuanzia 2004 hadi 2017 si mchezo.

Ndiyo maana baada ya uvumi kuanza kuenea hivi karibuni, kuna mgogoro ndani ya TFF unaomhusisha Wambura na matumizi mabaya ya TFF nilishtuka na kujiuliza kulikoni Wambura arudi katika matatizo yaliyomtenga na uongozi wa soka.

Kwa namna ambavyo amekuwa nje niliamini huu ni wakati wake wa kukifanya kile alichokuwa akikipigania kwa miaka zaidi ya 10 yaani kuhakikisha anaongoza na kuchangia mafanikio ya soka la Tanzania lakini kilichotokea ni tofauti.

Wambura sasa anarudi katika vita ile ile ya nje ya uwanja baada ya kufungiwa maisha kujihusisha na soka akituhumiwa kwa makosa anayodaiwa kuyafanya mwaka 2013 wakati huo akiwa si kiongozi TFF. Mjadala mkubwa uliotawala vichwa vya wadau wa soka ni hoja ya kama Wambura ameonewa au alichofanyiwa ni sahihi? Kumwadhibu kiongozi kwa tuhuma zinazofanyiwa kazi na vyombo vya sheria na ambazo hazijafikishwa mahakamani ni kumwonea.

Nimewahi mara kadhaa kuwasikia wanasheria wakiutumia msemo wa “A person is innocent until proven guilty” kwamba mtu yeyote si mkosaji hadi hapo itakapothibitishwa amefanya kosa (tafsiri yangu).

Kwa hiyo Wambura alitakiwa asubiri uchunguzi wa vyombo vya sheria ndipo aadhibiwe au TFF wangempeleka mahakamani na kama mahakama ingemwona na hatia ndipo TFF wangekuwa sahihi kutoa adhabu yao ya kifungo cha maisha kwa Wambura.

Wakati Rage akiwa Katibu wa FAT, waziri aliyekuwa na dhamana ya katika michezo, Profesa Juma Kapuya aliunda tume kuchunguza ubadhirifu wa mali za FAT, tume hiyo chini ya Jenerali Ulimwengu ilibaini kuwapo matumizi mabaya ya mali za FAT.

Pamoja na hilo hakuna kiongozi wa FAT aliyesimamishwa au kufungiwa na hata suala hilo lilipofikishwa mahakamani bado Rage aliendelea na kazi yake ya ukatibu kama kawaida, alibaki kuwa mtuhumiwa na si mkosaji, mifano ipo mingi tu. Pengine hapo ndipo unapoweza kujiuliza kwa nini kwa Wambura imekuwa tofauti?

Je kilichofanywa ni mkakati kama ambavyo Wambura mwenyewe anavyolalamika, Rais wa TFF, Wallace Karia na timu yake walikuwa na mkakati wa kumtoa kafara Wambura, mkakati ambao wameufanikisha? Hata hivyo, kwa upande mwingine nimewahi kuwasikia wanasheria hao hao wakisema; A person is guilty until proven innocent ‘Mtu ni mkosaji hadi hapo itakapothibitisha si mkosaji (tafsiri yangu).

Nimeambiwa usemi au utaratibu huu unatumiwa sehemu nyingi tu, lakini zaidi inatajwa nchi ya Ufaransa na hata hivi karibuni kwa aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma alishinikizwa kujiuzulu kwa tuhuma zilizomkabili bila hata mahakama kumkuta na hatia.

Usemi huu wa pili unaitoa TFF katika kosa, Rais Karia na timu yake wapo sahihi kwa hatua walizomchukulia Wambura na ni jukumu la Wambura kupambana kusafisha jina lake ili arudi tena kwenye uongozi wa TFF. Zaidi ya hilo, Wambura amewahi kuitafuta haki yake akiwa nje, akiwa Katibu Mkuu FAT aliwahi kusimamishwa na Kamati ya Utendaji kwa kosa la kushindwa kuwasilisha jina la timu ya Tanzania iliyopaswa kushiriki mashindano yanayoandaliwa na CAF.

Wambura akiwa ndiye Katibu Mkuu alidaiwa kuzembea na hivyo akaadhibiwa, aliikubali adhabu hiyo akapambana kuisaka haki yake nje ya uongozi, akaipata na kurudi katika nafasi yake ya ukatibu mkuu japo tofauti ni kwamba wakati ule aliadhibiwa na kamati ya utendaji.

Pia ikumbukwe tuhuma zinamchafua mtu na kwa wasiopenda kuchafuliwa inapotokea hali hiyo huamua kukaa pembeni ili wachunguzwe.

Kwa hiyo wadau wa soka hawana sababu ya kulumbana, Wambura bado ana nafasi ya kuitafuta haki yake na naamini akiitafuta hata nje ataipata kwani amewahi kufanya hivyo.

Hata hivyo, lazima ajiangalie mwenyewe kwanza na kujiridhisha hajahusika kwa lolote katika kashfa anazohusishwa nazo, hajaghushi chochote na kupokea fedha Sh84 milioni isivyo halali kama ambavyo imeelezwa, tofauti na hivyo atajiingiza katika matatizo zaidi.

Kwa maana nyingine, sakata hili linaweza kumfanya aibuke shujaa au kumzamisha zaidi na kumwondoa maisha katika soka kwa kuzingatia adhabu aliyopewa.