Walahi msiogope!

Muktasari:

  • Mabosi hao wa Yanga wamelazimika kufanya hivyo baada ya kugundua kuwa watani zao Simba waliwahi mapema visiwani hapa wakiongozwa na Makamu wao wa Rais, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, Katibu Mkuu, Patrick Kahemele na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Mohammed Kigoma.

KATIKA siku ambazo Kamati ya Mashindano ya Yanga ilikuwa na mishemishe ni juzi Jumapili na jana Jumatatu. Vigogo wa kamati hiyo na viongozi wengine walishuka kwa wingi mjini hapa si tu kutokana nakipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Azam.

Bali baada ya kuthibitika rasmi kwamba wanavaana na Mnyama leo Jumanne mida ya Saa 2:15 usiku mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi, Yanga wanapambana kuhakikisha wanapandisha morali ya wachezaji wao na kupanga mikakati ya karibu na benchi la ufundi, ili kuhakikisha mambo yanakwenda sawa, haswa kutokana na mzuka mkubwa walionao Simba ambao hawajapoteza mchezo na straika Laudit Mavugo amerudi kwenye fomu.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Yanga, Samuel Lukumay alikuwepo visiwani hapa tangu mechi na Azam sambamba na mdau mkubwa wa timu hiyo, Omary Chuma lakini jana Jumatatu vigogo wengine, Abdallah Bin Kleb na Seif Ahmed ‘Seif Magari’ walitua.

Mabosi hao wa Yanga wamelazimika kufanya hivyo baada ya kugundua kuwa watani zao Simba waliwahi mapema visiwani hapa wakiongozwa na Makamu wao wa Rais, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, Katibu Mkuu, Patrick Kahemele na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Mohammed Kigoma.

Kukamilika jopo hilo la viongozi kunatarajiwa kuongeza msisimko wa mchezo wa watani wa jadi Simba na Yanga visiwani hapa wakiwa wanakutana mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Amani, tangu 2011 ambapo Simba ilishinda kwa mabao 2-0 kwenye mchezo wa fainali.

Simba inaingia katika mchezo wa leo ikiwa imefanya vizuri zaidi katika hatua ya makundi, ilizifunga Taifa mabao 2-1, KVZ bao 1-0 na Jang’ombe Boys mabao 2-0 huku ikitoka sare tasa na URA ya Uganda.

Awali kabla ya kipigo kutoka Azam, Yanga ilizifunga Jamhuri ya Pemba mabao 6-0 na Zimamoto mabao 2-0.

Tathmini inaonyesha kuwa matokeo ya mechi za makundi yameifanya Simba kuwa timu inayojiamini zaidi katika mechi hiyo tofauti na Yanga ambayo imekuwa na unyonge kutokana na kupoteza mchezo wa mwisho dhidi Azam.

KAULI ZA MAKOCHA

Vigogo wa Yanga wamewaondoa hofu mashabiki na hata Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alikiri kuwa timu yao ilifanya makosa katika mchezo na Azam, hivyo wanafanya kazi kubwa kurekebisha makosa yao ili yasijirudie katika mchezo na Simba na mashabiki wasiogope waje uwanjani kwa kujiamini kuishangilia timu yao.

“Tulifanya makosa dhidi ya Azam na wakatuadhibu, tunatazama mbele sasa kurekebisha makosa, ili tuweze kupata ushindi katika mechi ya nusu fainali,” alieleza Mwambusi mmoja mwa makocha wazawa wanaoheshimika.

“Kimsingi, tulipokuja katika mashindano tulijiandaa na mechi zote hivyo kukutana na Simba siyo habari ya kushtua, kwetu haijalishi tunakutana na nani kwani tuko makini,” alifafanua kocha huyo wa zamani wa Mbeya City na Moro United.

Jackson Mayanja ambaye ni Kocha Msaidizi wa Simba ameonekana kujiamini zaidi kuelekea katika mchezo huo, huku akidai kuwa msimu huu wana timu nzuri na Yanga lazima aumie na akawasisitizia mashabiki wa Msimbazi waje kwa mbwembwe zote.

“Siwezi kusema kuwa ni safu ya ulinzi pekee itakayotusaidia kufanya vizuri dhidi ya Yanga, ni kweli inacheza vizuri, lakini tuna timu nzuri ya kupata ushindi katika mchezo huo,” alisema Mayanja.

“Tumejiandaa vizuri tangu mwanzo na tunategemea utakuwa mchezo wenye ushindani mkubwa. Kwetu hatuogopi timu wala mechi kwa kuwa lengo letu ni ubingwa, tutacheza aina yetu ile ile ya soka la kukaba na kushambulia kwa pamoja,” alifafanua.

MAKOCHA WENGINE

Kocha Msaidizi wa URA, Massa Simeone alisema utakuwa ni mchezo wenye uzani sawa kwani timu zote mbili zimeonyesha kiwango cha kuvutia katika michuano hii ya Mapinduzi.

“Zote ni timu nzuri, nategemea utakuwa ni mchezo wenye ulingano hasa kutokana na ukweli kwamba wote wameonyesha viwango vya kuvutia,” alisema.

“Hata hivyo kila timu ina nguvu na mapungufu yake, Simba ni nzuri sana katika eneo la ulinzi, ni ngumu kuivunja safu yao ya ulinzi na kupata bao. Yanga ni wazuri katika eneo la ushambuliaji, wanakuwa hatari sana kwenda mbele ila katika ulinzi si imara sana,” alieleza kocha huyo.

Kocha Mkuu wa Jang’ombe Boys, Mohammed Seif ‘King’ alisema mara nyingi mchezo wa Simba na Yanga hauna ufundi mwingi kutokana na timu hizo kujuana na kufahamu namna ya kucheza wenyewe kwa wenyewe.

“Mechi za Simba na Yanga tuwaachie tu wenyewe, huwezi kusema kiufundi timu itachezaje kwani wenyewe wanajuana na mechi zao huwa zinahusisha timu nyingi,” alieleza King ambaye aliipandisha Azam ligi kuu mwaka 2008.

MBINU ZA MAKOCHA

Kocha wa Yanga, George Lwandamina bado ana ugeni na timu hiyo ambapo amekuwa akitumia silaha kubwa ya kuwataka wachezaji wake wakabe kuanzia eneo la mpinzani. Katika mfumo huo kuanzia straika hadi beki wote wanakaba na kushambulia.

Lwandamina amekuwa akiwategemea mawinga wake, Saimon Msuva na Emmanuel Martin kupeleka mashambulizi kupitia pembeni, huku Haruna Niyonzima akicheza huru kama namba 10 nyuma ya straika ili kuongeza ubunifu katika eneo la mbele.

Yanga ikicheza kwa kutumia mbinu hiyo imekuwa hatari na mara nyingi inainyima uhuru timu pinzani ambayo hulazimika kutegemea mashambulizi ya kushtukiza pekee.

Kocha Joseph Omog amekuwa akiamini katika kuubana uwanja kwa timu yake kucheza zaidi katikati, huku akitegemea mashambulizi ya pembeni kupitia upande wa kushoto kwa Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

Katika mchezo wa leo Omog anatarajia kutumia viungo watatu ambapo Jonas Mkude, Mzamiru Yassin watacheza sambamba na Mwinyi Kazimoto ama James Kotei. Omog amekuwa akimtumia pia kiungo mshambuliaji, Mohammed Ibrahim kama straika kivuli.

YANGA MBELE, SIMBA NYUMA

Timu hizi zinakutana kila moja ikiwa na silaha yake ya pekee ambapo Yanga inasifika kwa safu imara ya ushambuliaji ikiwa imefunga mabao nane katika mechi tatu za mwisho wakati ambapo Simba imefunga mabao matano katika mechi nne za mwisho.

Washambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe, Saimon Msuva, Donald Ngoma ambaye hatacheza leo kutokana na maumivu ya goti wamekuwa hatari na vigumu kuzuilika. Hata hivyo Yanga tayari imeruhusu mabao manne katika michuano hiyo.

Simba licha ya safu yake ya ushambuliaji kusuasua imekuwa imara katika safu ya ulinzi ikiwa imeruhusu bao moja pekee katika mechi nne za michuano hiyo. Safu ya ulinzi ya Simba inayoundwa na Janvier Bokungu, Method Mwanjali, Abdi Banda na Tshabalala imekuwa imara na ngumu kupenyeka.

Hata hivyo changamoto kubwa ya Simba itaendelea kuwepo katika safu ya ushambuliaji ambapo mastaa wake, Laudit Mavugo, Juma Liuzio, Pastory Athanas na Mohammed Ibrahim wamekuwa hawana makali ya kutisha.

Mavugo ambaye alifunga mabao mawili katika mchezo wa mwisho dhidi ya Taifa Jang’ombe, alisema anafurahi kuweza kuyapata makali yake kabla ya mechi ya Yanga kwani imempatia hali ya kujiamini.

“Nashukuru nimefunga wakati ambapo tunaelekea katika mchezo muhimu na Yanga. Huwa inatokea kiwango kinashuka na kupanda lakini sasa nimepata hali ya kujiamini na ninatazama mbele kufunga zaidi,” alisema straika huyo.

AZAM NA JANG’OMBE

Mechi ya kwanza leo jioni Azam itacheza na Taifa Jang’ombe katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali. Azam ilimaliza kama vinara wa Kundi B hivyo kukutana na Taifa ambayo ilimaliza ya pili katika Kundi A.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa na msisimko mkubwa kutokana na timu ya Taifa kuwa na mashabiki wengi visiwani hapa huku Azam ikipata umaarufu mkubwa baada ya kuifunga Yanga katika mchezo wao wa mwisho hatua ya makundi.

Kocha wa muda wa Azam, Idd Nassor ‘Cheche’ alisema lengo lao ni kutwaa ubingwa hivyo wataingia katika mchezo huo kwa nguvu zote kama walivyofanya katika mechi ya mwisho na Yanga.

VIKOSI VIPO HIVI;

SIMBA:

Peter Manyika, Janvier Bokungu, Mohammed Hussein, Abdi Banda, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Muzamir Yassin, Laudit Mavugo, Juma Liuzio na James Kotei.

YANGA:

Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Kelvin Yondani, Andrew Vincent, Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Haruna Niyonzima na Emmanuel Martin.