Wambura awapa neno wakufunzi wa waamuzi Afrika

Muktasari:

Wambura alisema hayo kwenye Ukumbi wa ILO jijini Dar es Salaam, alipokuwa anafungua kozi ya wakufunzi wa waamuzi kutoka sehemu mbalimbali barani Afrika.

Makamu Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Michael Wambura amesema, kuna uwezekano mkubwa Bara la Afrika, likatoa idadi kubwa ya waamuzi katika fainali za michuano mikubwa hususani Kombe la Dunia.
Wambura alisema hayo kwenye Ukumbi wa ILO jijini Dar es Salaam, alipokuwa anafungua kozi ya wakufunzi wa waamuzi kutoka sehemu mbalimbali barani Afrika.
Kozi hiyo ambayo ni ya wiki moja kwa wakufunzi wa waamuzi hatua ya tatu ‘Futuro III’ inafanyika Tanzania na imeshirikisha jumla ya washiriki 58 kutoka nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania.
Kozi hiyo ina wakufunzi sita wakiwamo Carlos Henriques na Dominic Chiellens wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), ambao Wambura aliwataka wakufunzi wanaofundishwa mbinu mbalimbali kufanya kazi kwa weledi ili kutimiza ndoto hiyo ya Afrika.
“Waamuzi wa Afrika wana uwezo. Ninyi wakufunzi ni wa kufanya waamuzi wetu kuwa na uwezo zaidi. Ni Aibu kwa Bara kubwa kama Afrika lenye nchi wanachama 54 wa FIFA kuwa na waamuzi wachache katika fainali za Kombe la Dunia.
“Tuazimie kuwa na waamuzi wa kutosha katika fainali kubwa kama hizo,” Alisema Wambura ambaye alipigiwa makofu na washiriki kwa kuwatia shime wakufunzi.