Wakongo wamtibulia usajili wa Bwalya kutua Simba

Muktasari:

Taarifa kutoka Zambia ni kwamba utata huo wa Bwalya anayekipiga katika klabu ya Nkana umeibuliwa na Chama cha Soka cha DR Congo (Fecofa) wakisema mshambuliaji huyo ni raia halali wa nchi yao na siyo Zambia.

Dar es Salaam. Mshambuliaji anayefanya mazungumzo na  Simba, Walter Bwalya amezusha utata mkubwa unaoweza kumsababishia kifungo kutoka Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) baada ya sintofahamu juu ya usahihi wa uraia wake.

Taarifa kutoka Zambia ni kwamba utata huo wa Bwalya anayekipiga katika klabu ya Nkana umeibuliwa na Chama cha Soka cha DR Congo (Fecofa) wakisema mshambuliaji huyo ni raia halali wa nchi yao na siyo Zambia.

Chama hicho kimetoa ushahidi wa viambatanisho wakisema Bwalya wakati akiwa Congo alikuwa akijulikana kwa jina la Binene Sabwa ambapo akiwa huko alichezea Lubumbashi Sport kabla ya kuhamia Forest Rangers ambayo nayo ilimuuza Nkana anayoitumikia mpaka sasa.

Tayari chama cha soka nchini Zambia (FAZ) kimeanza kuchunguza sakata hilo kwa kumuhoji Bwalya ilkuaje akacheza soka nchini kwao bila ya kuwa na Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ambapo huenda hatua hiyo ikampotezea dili la kutua Simba.

Bwalya anayejua vyema kufunga kwa mguu wake wa kushoto, yumo katika orodha ya washambuliaji wanaotakiwa na Simba msimu huu sambamba na Donald Ngoma wa Yanga ambapo sakata hilo limemsababishia klabu yake Nkana kutomchezesha katika mchezo wa ligi juzi Juni 24 wakati wakiichapa Buildcon kwa bao 1-0.