Wakongo wa russia 2018

Muktasari:

Kwa bahati mbaya nchi hiyo imeshindwa kufuzu kwa fainali hizo kubwa kabisa za soka duniani na mastaa wake wanazinufaisha nchi nyingine kwenye ulingo wa soka la kimataifa.

MOSCOW, RUSSIA. VIPAJI vingi sana vinavyotesa kwenye soka la Ulaya na hasa kwenye timu za taifa za nchi za Ufaransa na Ubelgiji, ambazo zinapewa nafasi kubwa ya kwenda kubeba ubingwa wa Kombe la Dunia huko Russia asili yao ni DR Congo.

Kwa bahati mbaya nchi hiyo imeshindwa kufuzu kwa fainali hizo kubwa kabisa za soka duniani na mastaa wake wanazinufaisha nchi nyingine kwenye ulingo wa soka la kimataifa.

Hii hapa orodha ya Wakongo ambao kwa asilimia 100 watakuwapo kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Russia kuwakilisha mataifa ya Ulaya.

Steve Mandanda (Ufaransa)

Mandanda ni bonge la kipa kwenye Ligue 1 akikipiga kwenye kikosi cha Olympique de Marseille na jina lake limetajwa kwenye orodha ya watakaokwenda kuiwakilisha Ufaransa kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia mwezi ujao.

Alizaliwa Kinshasa na ana wadogo zake watatu ambao pia ni makipa Parfait, kipa wa Charleroi na Timu ya Taifa ya DR Congo; Riffi, kipa wa AC Ajaccio na timu ya vijana ya Ufaransa U-16; na Ever, ambaye ni kipa Lusitanos Saint-Maur.

Vincent Kompany (Ubelgiji)

Vincent Kompany ni beki wa kati wa Timu ya Taifa ya Ubelgiji na bila ya shaka atakuwapo kwenye fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazofanyika Russia kuanzia mwezi ujao.

Beki huyo ni nahodha wa timu hiyo na kwenye klabu yake ya Manchester City pia ya England. Baba yake Kompany, Pierre ni Mcongo, aliyehamia Ubelgiji na amekuwa wakala wa mchezaji huyo. Mama yake, Kompany, Jocelyne, ndiye Mbelgiji. Kutokana na hilo, Kompany aliamua kufuata upande wa mama na kuitumikia Timu ya Taifa ya Ubelgiji, ambayo imesheheni mastaa wa maana.

Steven N’Zonzi (Ufaransa)

Steven N’Kemboanza Mike Christopher N’Zonzi alizaliwa katika mji wa Colombes huko Ufaransa na wazazi wa kutoka DR Congo. Angeweza kufuzu kuichezea timu ya taifa ya nchi hiyo ya Afrika, lakini mambo yalikuwa tofauti na mwaka 2009 alichaguliwa kuichezea Timu ya Taifa ya Vijana ya Ufaransa kwa U-21. Mwaka 2011 aligoma kwenda kuichezea DR Congo kutokana na matatizo ya kiutawala na hapo akashindwa kuichezea timu hiyo.

Mwaka uliofuatia Wakongo walihitaji akacheze kwenye timu yao, N’Zonzi akakataa tena na sasa utamuona huko Russia akiwa na jezi za Les Bleus.

Romelu Lukaku (Ubelgiji)

Straika wa Manchester United, Romelu Menama Lukaku Bolingoli alizaliwa huko Antwerp, mji uliopo Kaskazini mwa Ubelgiji. Lakini, wazazi wake Lukaku ni Wakongo. Baba yake, Roger Lukaku, aliichezea Zaire kipindi hicho ambapo kwa sasa ndiyo inayofahamika kama DR Congo. Lakini, fowadi huyo aliyenaswa kwa Pauni 75 milioni na Man United mwaka jana akitokea Everton aliamua kuitumikia Ubelgiji kwenye soka la kimataifa. Alianza kucheza soka la kimataifa kwenye kikosi cha Ubelgiji mwaka 2010 na tangu wakati huo hadi sasa ndiye kinara wa mabao kwenye kikosi hicho chenye mastaa kibao akiwamo Eden Hazard na Kevin De Bruyne.

Blaise Matuidi (Ufaransa)

Kiungo wa Juventus na Timu ya Taifa ya Ufaransa, Blaise Matuidi alizaliwa Toulouse, Haute-Garonne. Baba yake, Faria Rivelino anatokea Angola na mama yake, Elise ni Mkongo. Rivelino alihamia Ufaransa akiwa mdogo na kufanikiwa kukutana na mrembo wa Kikongo, Elise ambaye alifanikiwa kupata mtoto huyo Matuidi anayekipiga huko Juventus.

Kiungo huyo wa kati kutokana na hilo angeweza kufuzu kuichezea DR Congo na Timu ya Taifa ya Angola, lakini aliamua kuitumikia Les Bleus na mwezi ujao utamuona kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia.

Christian Benteke (Ubelgiji)

Huduma yake kwa sasa anaitoa huko kwenye kikosi cha Crystal Palace. Ni bonge la mshambuliaji na kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia atakuwa ndani ya uzi wa Kibelgiji.

Benteke, historia yake inaonekana alizaliwa Kinshasa huko DR Congo mwaka 1990 na familia yake ilikimbilia Liege, Ubelgiji mwaka 1993. Alianza kucheza timu ya taifa ya Ubelgiji 2007 akianza na U-17.