Wakenya wavuta pesa ndefu Marathon

Wednesday November 8 2017

 

By THOMAS MATIKO

MSIMU huu umeendelea kuwa mzuri kwa mastaa wa Marathon wa humu nchini. Hii ni baada ya nyota wawili Geoffrey Kamworor na  Wilson Kipsang, kuvuta za maana juzi Jumapili kwenye makala ya 48 ya New York Marathon.

Kamworor 24, aliunda dola 100,000 (Sh10 milioni) kwa kushinda mbio hizo huku Kipsang, 35, akilambishwa dola 60,000 (Sh6 Milioni) kwa kumaliza wa pili.

Hata hivyo, nyota hao walikosa bonasi zaidi kwa kukimbia nje ya muda wa saa 2:10 ambao, kama wangefanikiwa wakijikusanyia kiasi zaidi ambacho hakingepungua dola 10,000.

Kamworor bingwa mara mbili wa mbio za nyika duniani ambaye miezi miwili kabla, alionya wapinzani wake kwamba watarajie ushindani mkali kutoka kwake, aliishia kutimiza kauli yake kwa kushinda mbio hiyo kwa muda wa saa 2:10.53.

Hazikuwa mbio rahisi sana kwake kutokana na ushindani aliokuwa nao huku akiamua kutumia mbinu za kijanja kuwatoa pale alipofyatuka kwa kiki zikiwa zimesalia kilomita 3 huku akiandamwa na Kipsang.

Nafasi ya pili ilichukuliwa na Kipsang mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia, ambaye pia ni bingwa wa Tokyo Marathon 2017.